1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Italia ajiuzulu

22 Februari 2007

Rais Giorgio Napolitano wa Italia ameanza majadiliano ya kutafuta serikali mpya baada ya nchi hiyo kufikwa na mashangao mkubwa pale waziri mkuu Romano Prodi alipotangaza kuwa amejiuzulu.

https://p.dw.com/p/CHJZ
Romano Prodi waziri mkuu wa Italia aliejiuzulu
Romano Prodi waziri mkuu wa Italia aliejiuzuluPicha: AP

Waziri mkuu wa Italia Romano Prodi alijiuzulu mara tu chama chake cha mfungamano wa mlengo wa kadiri wa kushoto kiliposhindwa katika kura ya baraza la seneti juu ya sera za mambo ya nje, kurefusha muda wa majeshi ya Italia nchini Afghanistan pamoja na kupanuliwa kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Italia.

Hali hiyo ilimlazimu rais Giorgio Napolitano kurukia kwenye mparaganyo huo ili kuokoa matukio ya kisiasa ya miaka ya themanini na tisini wakati ambapo Italia ilishuhudia wimbi la kubadilika serikali mara kwa mara kila baada ya kipindi cha muda wa wiki chache tu.

Kelele zilipigwa baada ya kutangazwa matokeo ya kura bungeni, upande wa upinzani ukisherehekea kwa sababu kura mbili tu zilipungua ili kuweza kurefusha muda wa majeshi ya Italia nchini Afghanistan.

Kabla ya kupigwa kura uongozi wa waziri mkuu Romano Prodi ulilazimika kujitetea juu ya pendekezo la kupelekwa wanajeshi 2000 kujiunga na kikosi cha kimataifa nchini Afghanistan na vilevile juu ya hatua ya kupanuliwa kambi ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Vicenza kaskazini mwa Italia.

Waziri wa mambo ya nje Massimo D’Alema katika utetezi huo alisema.

Ili kuzikabili changamoto za Afghanistan inalazimu kushiriki zaidi katika kuiimarisha nchi hiyo kisiasa na kiuchumi.

Sera hizo zilipingwa vikali na vyama vya mlengo wa shoto vya Greens na Kikomunisti vilivyo ndani ya mfungamano wa chama tawala.

Wapinzani wa kihafidhina ndio hasa waliomtaka waziri mkuu Romani Prodi afunge virago vyake baada ya mswaada wake kushindwa bungeni.

Serikali ya waziri mkuu Romano Prodi ilihitaji kura 160 za baraza la seneti ili kuibuka mshindi lakini badla yake ni maseneta 158 pekee ndio waliouunga mkono mswaada wa Romano Prodi huku maseneta 136 wakiupinga na kuifanya serikali ipoteze kura hiyo muhimu.

Ijapokuwa kura hiyo haikuwa rasmi juu ya kuwa na imani na serikali ya waziri mkuu Romano Prodi lakini waziri wa mambo ya nje wa Italia alikuwa tayari ameshabashiri kuwa utawala wa Prodi lazima unga’atuke iwapo mswaada wake ungeshindwa.

Takriban watu alfu 80 walishirki katika maandamano mwishoni mwa wiki kupinga upanuzi wa kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Italia.

Rais Giorgio Napolitano wa Italia sasa yumo katika harakati za kufanya mazungumzo na vyama mbali mbali lakini hata hivyo anaweza kumchagua tena Romano Prodi katika wadhifa huo huo wa waziri mkuu au kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mkuu mpya.