1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Italia kujiuzulu mwishoni mwa mwezi huu

9 Novemba 2011

Waziri mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, leo amesema atajiuzulu ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao. Berlusconi aliyasema haya katika mahojiano na kituo kimoja cha habari nchini humo.

https://p.dw.com/p/137FV
Waziri mkuu wa Italia Silvio BerlusconiPicha: dapd

Waziri mkuu huyo wa Italia amesema atajiuzulu punde tu bunge litakapoidhinisha sheria ya kufufua uchumi wa nchi hiyo, jambo linalotarajiwa kufanyika mwezi huu. Mauzo katika soko la hisa ya italia leo yalifunguliwa kwa asilimia 1.38 juu baada ya taarifa ya kujiuzulu kwa Waziri mkuu huyo.

Tangazo la kujiuzulu kwake limeiweka Italia katika mkwamo wa kisiasa kutokana na hofu kuwa nchi hiyo ya Ulaya ya tatu tajiri kiuchumi huenda ikaathirika na mzozo wa madeni ya Ulaya. Uchumi wa Italia umeathirika vibaya kutokana na mzozo wa madeni unaokumba mataifa yanayotumia sarafu ya Euro.

EU Finanzminister Brüssel
Wanachama wa umoja wa ulaya.Picha: dapd

Kundi la Umoja wa Ulaya lipo nchini Italia kuangalia marekebisho ya maswala muhimu ya uchumi baada ya umoja huo na shirika la kimataifa la fedha duniani, IMF kuiweka nchi hiyo katika uwazi wa kuichunguza juu ya mpango wake wa kuinua uchumi.

Magazeti nchini humo yanasema hatua hii ya mvutano wa polepole wa maswala muhimu ya Italia inaweza kuiweka nchi hiyo inayogubikwa na msukosuko wa kiuchumi kwa miezi kadhaa sasa katika matatizo makubwa ya kifedha.

Gazeti la Leftist daily La Repubblica pia limeandika habari chungu nzima juu ya hatua ya Berlesconi kujiuzulu. Gazeti hilo limesema italia bado inaweza kunusurika iwapo Waziri mkuu huyo ataachia madaraka mara moja, kwa kuwa tayari ameshaonesha mapungufu yake katika kushughulikia swala muhimu la msukosuko wa kiuchumi unaoikumba nchi hiyo kwa sasa.

Njia mojawapo iliopendekezwa ya kufufua uchumi wa nchi hiyo ni kuipanua serikali ya sasa ya mseto baina ya vyama vya mrengo wa kati na kulia, kiongozi mpya akitokea  chama cha Berlusconi, au kuundwa serikali ya Umoja wa Taifa itakayoongozwa na stadi wa mamboy a uchumi. .

Lakini bwana Berlusconi amepinga hilo. Amesema kwa maoni yake kufanyika uchaguzi ndio njia pekee ya nchi hiyo kupiga hatua.

Berlusconi amekuwa mtu muhimu katika siasa ya Italia katika muda wa miongo miwili, na hivi karibuni aliponea chupuchupu kura 50 za kutokuwa na imani naye. Berlusconi, waziri mkuu aliyeongoza kwa miaka mingi nchini Italia, anakumbwa na misururu ya sakata za kisheria na  kashfa za ngono, pamoja na migororo ya kisiasa na kiuchumi. Hata hivyo rais wa Italia Giorgio Napolitano, anatarajiwa kuwa na mazungumzo na maafisa wake wa kisiasa juu ya swala hilo.

Kutokana na italia kuwa na deni kubwa la trillioni 2.6 imewapa hofu kubwa wawekezaji nchini humo kuwa Italia iko njiani kuelekea katika mzozo wa madeni ya ulaya.

Mwandishi Amina Abubakar/AFPE

Mhariri Othman Miraji