1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa ulinzi wa Marekani akaribishwa Iraq na milipuko ya mabomu

Siraj Kalyango5 Desemba 2007

Marekani haibanduki kutoka Iraq hata baada ya 2008

https://p.dw.com/p/CXXI
Robert Gates,waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani

Waziri wa Ulinzi wa Marekani amefanya ziara ya ghafla nchini Iraq.Ziara hii ina nia ya kuwa himiza viongozi wa nchi hiyo kuchapuza harakati za maridhiano kufuatia kupunguka kwa visa vya ghasia katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na mauaji kwa mda mrefu .

Aidha imefanyika wakati serikali ya Czech imeamua kuviondoa vikosi vyake huko.

Ziara ya sasa ya waziri,Robert Gates,wa Marekani,haikutangazwa hapo kabla labda kwa sababu za kiusalama.

Na imekuja wiki moja Unusu, baada ya makubaliano ya rais George W. Bush wa Marekani na waziri Mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki, kuhusu mpango wa kuyaweka majeshi ya Marekani nchini Iraq kwa mda mrefu hata kupita mwaka ujao wa 2008.

Afisa wa habari wa wizara ya Ulinzi ya Marekani, amenukuliwa kusema kuwa ,waziri Gates yuko Iraq kujionea mwenyewe maendeleo yaliyofikiwa tangu safari yake ya mwisho nchini humo iliofanyika karibu miezi mitatu iliopita.

Afisa huyo anaendelea kuwa miongoni mwa wengine atakaokutanao ni rais wa Iraq, Jalal Talabani.

Aidha waziri huyo anatarajiwa kuuhimiza uongozi wa Iraq, kupasisha haraka miswada miwili muhimu yenye lengo la kuboresha maridhiano hasa wakati huu ambapo wanasema kuwa ghasia zinapungua.

Miswaada inayosemwa ni ile kuhusu maridhiano, mkataba kuhusu nishati na sheria kuwahusu wanachama wa zamani wa chama cha Saddam Hussein cha Baath.

Washington inaona kuwa kupasishwa kwa miswaada hiyo na hatimae kuwa sheria,hasahasa ile miwili ambayo imekwamia bungeni, kutawashawishi waaraba wa kiSunni kuacha mwelekeo wao wa kuwaunga mkono wapiganaji wa chini kwa chini wanaopinga kuweko kwa Marekani katika nchi hiyo.

Tena ule muswaada wa nishati unahusu mafuta na gesi.

Sheria itasaidia kuhakikisha kuwa mapato kutokana na mauzo yanagawiwa sawa baina ya mikoa yote 18 ya Iraq.WaSunni walikuwa wanaogopaWakurdi pamoja na waShia ndio watakuwa na ukiritimba wa mapato hayo.

Sheria kuwahusu wanachama wa zamani wa chama cha Baath,itawahusu maaofisa hao wa ngazi za kati ambao hawakuhusika na maovu ya utawala uliopita.

Waziri Gates bila shaka hatalipa kisogo suala la wafungwa walioko katika gereza zinazosimamiwa na Marekani nchini Iraq.

Kuna wa Iraq wanaofikia elf 26,katika jela hizo na wengi wao ni wa Sunni.

Ziara ya waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini humo wakati maofisa wa Marekani na Iraq wakidai kupungua kwa visa ghasia kufuatia operesheni safisha ya vikosi vya Marekani ilioanzishwa Febuari mwaka huu.

Mapema mwezi huu,mawaziri wa tatu wa Iraq walisema kuwa idadi ya vifo vya waIraki imepungua wakati huo ikilinganishwa na mwezi wa Novemba ambapo inasemekana waliuliwa raia 606 wakiwemo na maofisa wa usalama.Mwezi Oktoba watu 887 ndio walikufa.

Hata hivyo,waziri wa Marekani, kwa sasa akiwa Baghdad lakini,amekaribishwa nchini humo na milipuko mitatu ya mabomu ambayo inasemekana imewauwa watu wanane.Milipuko hiyo ya magari imetokea katika mji wa Mosul ambako alifikia akitokea Afghanistan .

Ingawa maofisa wa Marekani na Iraq wanasema ghasia zimepungua lakini katika mwezi uliopita, Bush alikubaliana na waziri mkuu wa Iraq kuhusu mpango wa kuyabakiza majeshi yake huko Iraq.

Mkataba huo utaendelea hadi mwaka wa 2008 na baada ya hapo kibali cha umoja wa mataifa kinachokubali majeshi ya kigeni kukaa nchini Iraq, kikimalizika mikataba mingine kati ya serikali hizo itafikiwa ili majeshi ya Marekani yaweze kubaki huko hadi mwaka wa 2009.

Wakati huohuo bunge la Jamhuri ya Czech limepasisha mpango wa serikali wa kuondoa vikosi vyake kutoka Iraq mwaka ujao. Wabunge 195 wamepiga kura, ambapo 129 waipigia kura ya ndio ilhali kupingwa na wabunge 45 na 21 kuususia.Hii inamaana kuwa askari wake 80 kati ya wote 100 wataondolewa.

Wanajeshi wa jamhuri ya Czech wako kusini mwa Iraq wakilinda kambi ya jeshi la Uingereza.Waziri wa mashauri ya kigeni wa jamhuri ya Czech, Karel SCHWARZENBERG amesema kuwa askari wake waliosalia 20 kazi yao itakuwa kutoa mafunzo kwa maofisa wa Iraq baada ya kuombwa na utawala wa Baghdad.