1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zawadi ya utafiti wa kisayansi-Ujerumani.

2 Desemba 2009

"Zukunftspreis "yatolewa leo.

https://p.dw.com/p/KnWJ

Baadae hii leo ,itatolewa nchini Ujerumani ile ilioitwa "Zukunftspreis"-zawaidi yenye lengo la kukuza na kutilia shime ushirikiano kati ya wanasayansi na wanauchumi humu nchini.Kwani, licha ya taftishi kubwa za kisayansi na uvumbuzi unaofanywa humu nchini , ni bidhaa chache tu zinazo zalishwa kutokana na taftishi na uvumbuzi huo.

Tatizo hili sasa, limetambuliwa tena tangu na wanasayansi,wanauchumi hata na wanasiasa ; na wameazimia sasa kurekebisha dosari hiyo ili ufundi unaotokana na taftishi za vyuo vikuu uwasilishwe masokoni.

Vyombo kama MP3-Player,mitambo ya Fax-Computa-Disc- ni mifano 3 ya teknolojia inayotumiwa leo kote ulimwenguni na ambayo, teknolojia yake imevumbuliwa Ujerumani. Bidhaa kutokana na teknolojia hiyo ,lakini zimeundwa nchi za nje na kuuzwa masokoni.Hiyo ni mifano 3 inayobainisha wazi kwamba, katika taftishi za kisayansi iko kileleni duniani,lakini mara nyingi haifanikiwi,utaalamu ilioupata kutoka taftishi zake za kisayansi kuzitumia kiuchumi.

Hali hii inathibitisha pia Bw. Hans-Jörg Bullinger, rais wa Jumuiya ya Fraunhofer-Gesellschaft kwa utafiti unaotumika kuunda zana.Anasema,

"Ukijiuliza jinsi gani utafiti wa kisayansi unashirikiana na viwanda,utakuta bado tuko nyuma sana."

Jumuiya ya Fraunhofer-Gesellschaft, inafanya utafiti wa uvumbuzi ili kutumiwa na viwanda na jamii.Ina maabara 80 mbali mbali kote nchini Ujerumani; na bajeti ya Euro bilioni 1.4 kwa mwaka. Sehemu kubwa ya fedha hizo, Jumuiya hiyo inavuna kutokana na mikataba inayopewa na viwanda na miradi inayofadhiliwa na umma.

Sehemu ya fedha zake pia hutolewa na serikali ya Shirikisho ya Ujerumani na zile za mikoa, ili kufanya utafiti na uvumbuzi ambao baada ya miaka michache , uweze kunufaisha viwanda na jamii kwa wakati muafaka.

Kwa mfano,Jumuiya hii, imejipatia mafanikio makubwa katika kuripoti haki-miliki zinazotokana na uvumbuzi wake .Lakini sio kila mara, hufanikiwa kuvishawishi viwanda na makampuni ya Ujerumani kuamini kuwa uvumbuzi wake huo, una thamani za kiuchumi ukigeuzwa bidhaa. Ufundi uliopelekea kuundwa chombo cha MP3-player, ulivumbuliwa kwenye maabara ya Jumuiya hii ya Fraunhofer-Gesellschaft.Lakini, ulipokamilika uvumbuzi huo,hakuna kiwanda au kampuni hata moja la Ujerumani, lililoamini juu ya ufanisi wake .

Viwanda vingi vikavumbua mitindo yao ya zana kama hiyo ambavyo vikitaka kuileta sokoni.MP3-player baadae, ikavuma kwa kishindo masokoni ulimwenguni,lakini kabla kufika hatua hiyo, ulipotezwa muda mwingi kuupigia upatu na kuutembeza masokoni uvumbuzi huo.

Mtayarishi: Ramadhan Ali

Mhariri:M.Abdul-Rahman