1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza La Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa

11 Juni 2010

Iran kuitafakari adhabu ya kifo kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18.

https://p.dw.com/p/NoBc
Mkutano wa upinzani nchini Iran, uliofanyika mwaka uliopita.Picha: AP

Iran imekubali kwamba itaichunguza upya sera yake ya kuwapa adhabu ya kifo vijana, sera inayoshutumiwa vikali, pamoja na kuwapa uhuru waandishi wa habari, na uhuru wa kujieleza na kukusanyika. Haya yanajiri baada ya Mataifa ya Magharibi kuitolea changamoto Iran kuhusu kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za kibinadamu katika mkutano wa baraza la Umoja huo la Haki za kibinadamu mjini Geneva.

Katika Mkutano huo wa kutafakari rekodi za Iran kuhusiana na masuala ya haki za kibinadamu- nchi za Magharibi ziliikabili Jamhuri hiyo ya Kiislamu kwa kuzuia ujumbe wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuzuru nchi hiyo, licha kwamba Iran ilidai inashirikiana kikamilifu na baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Audioslideshow Iran Proteste 2009 10(11)
Ghasia za uchaguzi nchini Iran, Juni 2009.

Hata hivyo, Afisa wa ngazi ya juu wa Iran alikuwa mwepesi wa kusema watalaamu hao watano wa Umoja wa Mataifa waliruhusiwa kuingia Iran, huku akiishtumu Marekani kwa kueneza uvumi kuhusiana na ushirikiano wa Iran.

Katibu Mkuu wa Baraza la Iran la haki za kibinadamu, Mohammed Javad Larijani, alisema Iran iko tayari kuzungumzia rekodi yake ya haki za kibinadamu, lakini mataifa ya magharibi yasifikiri Jamhuri hiyo ya Kiislamu itaruhusu mienendo ya Kimagharibi nchini humo.

'' Sisi tumekomaa kimdemokrasia, sisi pengine ndio demokrasia kubwa kabia Mashariki ya Kati. Hivyo tunajivunia tena sana rekodi yetu ya Haki za Kibinadamu. Ndivyo Larijani alivyoliambia baraza hilo la Haki za kibinadamu la Umoja wa Mataifa.

Baraza hilo, lenye wanachama 47, kwanza lilianza kuipigia darubini rekodi ya Iran kuhusiana na haki za kibinadamu mwezi Februari, wakilenga zaidi madai ya adhabu za kifo pamoja vitendo vya mateso, kufuatia uchaguzi wa rais wa Juni mwaka uliopita.

Mjadala huo mjini Geneva ulifanyika siku moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha vikwazo vipya dhidi ya Iran, kuiadhibu kwa sababu ya mradi wake wa nyuklia.

Flash-Galerie Morgengymnastik im Iran
Mataifa ya Magharibi yanaishtumu rekodi ya Iran y ahaki za binadamu.Picha: Mehr

Kupigiwa huku kwa darubini kwa haki za kibinadamu nchini Iran pia kunafanyika wakati Upinzani nchini Iran umefutilia mbali mkutano wake mkubwa uliokuwa ufanyike kesho kuadhimisha mwaka mmoja tangu kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo uliokuwa na utata- wakidai wanahofia maisha yao, iwapo vikosi vya serikali vitakabiliana na wafuasi wa upinzani.

Kuhusiana na wito uliotolewa na mataifa kumi ya Ulaya kwa Iran kufutilia mbali adhabu ya kifo kwa vijana walio na chini ya umri wa miaka 18- Jibu la Iran ilikuwa kwamba itatafakari wito huo na imetilia maanani mapendekezo hayo. Iran, hata hivyo, ilisisisitiza umri uliowekwa wa mtu kuadhibiwa unatokana na mafungamanisho ya sheria ya dini ya Kiislamu.

Mwandishi: Munira Muhammad/ RTRE

Mhariri: Othman Miraji