1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bush na tishio la vita vikuu vya tatu vya dunia

18 Oktoba 2007

Maneno ya rais Bush wa Marekani ya kuonya kutokea vita vikuu vya tatu vya dunia, leo hii yanagonga vichwa vya habari. Licha ya kwamba bado hakuna ushahidi wowote Iran imefika wapi katika mradi wake wa kinyuklia, hata hivyo habari pekee kuwa Iran huenda itaweza kutengeza bomu la kinyuklia inawatia hofu Wamarekani. Ufuatao ni uchambuzi wa Peter Philipp juu ya onyo la rais Bush:

https://p.dw.com/p/C7hC

Hata si zaidi ya miaka mitano iliyopita pale rais Bush alipolenga jina lake liandikwe katika vitabu vya historia kwa kutangaza kwamba anataka kurudia mafanikio ya vita vya pili vya dunia barani Ulaya, yaani kuleta demokrasia na Uhuru katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kumangusha madarakani Saddam Hussein wa Iraq. Leo lakini, kila siku habari zinazosikika kutoka Iraq zinatuonyesha kwamba Marekani ilishindwa kutekeleza ndoto hiyo. Iraq haina uhuru wala demokrasia, wala hakuna nchi yoyote nyingine katika eneo hilo ambayo iligeuka kwa njia ya kidemokrasi na uhuru. Huko Marekani, watu wengi wanatambua hali halisi na wanatafuta namna ya kuondoka kwa haraka kutoka Iraq bila ya kuharibu heshima ya jeshi.

Bush ni mmoja kati ya walio wachache wanaoshika sera hizo hizo za miaka mitano iliyopita. Sasa Bush hata amesema Iran izuiliwe kujipatia silaha za kinyuklia, la sivyo vita vikuu vya tatu vya dunia vitaweza kuanzishwa.

Japokuwa wakati huo huo Bush alisema ataendelea na juhudi zake za kisiasa kuishinikiza Iran iachane na mradi wa kinyuklia, hakuna hata mtu mmoja ambaye anamuamini tena. Bush ni kama injini ya kampeni ya kimataifa dhidi ya sera za kinyuklia za Iran. Katika miaka ya nyuma mara nyingi alitishia kwamba anataka serikali ibadilishwe, hata ikiwa itakuwa lazima kutumia nguvu. Kwa vyoyote vile, Iran isimamishwe, alisema Bush.

Mpaka leo lakini Bush hajatoa ushahidi wa madai yake dhidi ya Iran, kwani ushahidi hamna. Kuna tuhumu tu kwamba kwa kupata utaaluma wa kinyuklia utaiwezesha Iran si tu kuutumia kutengeza nishati bali pia kujenga mabomu ya kinyuklia. Hiyo lakini ni hoja dhaifu sana ambayo haipaswi kuwa msingi wa kampeni ya kisasa itakayotumika kuanzisha vita vipya. Rais Bush, kwa upande wake, hafikirii wasiwasi huo, kwani yeye anajiamini kabisa.

Tusidharau kwamba Bush hayuko peke yake kwenye msimamo huu. Karibu wanasiasa wote wa Marekani ambao walianzisha kampeni yao ya uchaguzi wa rais walionya dhidi ya Iran na wanaahidi kwamba wataizuia Iran kutengeza silaha za kinyuklia. Hususan ikiwa wanazungumza mbele ya jumuiya za Wayahudi suala hilo hutajwa. Bush pia aliweka wazi msingi wa sera zake pale aliposema kuwa Iran ni adui mkubwa zaidi wa Israel inayotaka kuiangamiza Israel, kwa hiyo inabidi kuisimamisha Iran.

Hata wataalamu wa kijeshi wa Marekani lakini hawakubaliani na Bush. Licha ya kampeni ya maneno dhidi ya Israel, bado Iran si hatari kubwa kwa Israel. Haya aliyasema jenerali mkuu wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, John Abizaid na aliongeza kusema hata ikiwa Iran itakuwa na silaha za kinyuklia, dunia itaweza kuvumilia.

Basi sababu ya rais Bush kutumia maneno makali na kuzungumzia vita vya tatu vya dunia hasa ni ziara ya rais Putin wa Urusi nchini Iran. Putin alisema kwamba Iran ina haki ya kutumia nishati ya kinyuklia kwa njia ya amani. Haya lakini ni kinyume kabisa na mkakati wa rais Bush.