1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaridhia kurejea mazungumzoni

15 Septemba 2009

Iran imeridhia kurejea katika meza ya mazungumzo na wawakilishi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ifikapo Oktoba Mosi.

https://p.dw.com/p/JgrC
Makao makuu ya IAEA Vienna, AustriaPicha: AP

Mkutano huo una azma ya kuishawishi Iran kuusitisha mpango wake wa nuklia ila bila ya kuiongezea mbinyo.Iran kwa upande wake inasisitiza kuwa mazungumzo hayo hayatauangazia mpango wake wa nuklia.Wakati huohuo Shirika la Atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA linaendelea kulalamika kuwa Iran inaendelea kukataa kuzithibitisha hati ilizowasilishiwa kuuhusu mpango wake huo.

Makubaliano hayo ya kuridhia mazungumzo ifikapo Oktoba Mosi yalifikiwa baada ya mwakilishi wa Umoja wa Ulaya Javier Solana kuwasiliana na msuluhishi mkuu wa Iran katika suala la nuklia Saeed Jalili.Hatua hiyo inatokea ikiwa ni siku chache baada ya Iran kuwasilisha mapendekezo mapya.

Beligen EU Präsidentschaft Schweden Carl Bildt
Waziri wa mambo ya nje wa Sweden Karl BildtPicha: AP

Kikao hicho cha Oktoba Mosi ambacho huenda kikafanyika Uturuki kina azma ya kuishawishi Iran kuusitisha mpango wake wa nuklia vilevile kutoiwekea mbinyo zaidi.Kulingana na Karl Bildt Waziri wa mambo ya nje wa Sweden iliyo mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya hatua hiyo pekee ni ishara nzuri,''Mkutano wenyewe ni ishara ila umuhimu wake bado haujajulikana.Tumeshasema kuwa endapo wako tayari kuyashughulikia masuala mengine ambayo yameorodheshwa kuhusiana na nuklia huenda tukatoa msaada wetu pia.''

Utafiti wa siri

Kwa upande wake Iran imeridhia kushiriki katika mazungumzo hayo yatakayowaleta pamoja mataifa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani ila kwa masharti kwamba mpango wake wa nuklia hautojadiliwa.Iran imekuwa ikishikilia kuwa mpango wake wa nuklia una azma ya kutengeza nishati ya nuklia wala sio silaha jambo linalokanushwa na Marekani.

IAEA Treffen in Wien Ali Asghar Soltanieh
Balozi wa Iran katika IAEA Ali SoltaniehPicha: AP

Kwa upande mwengine shirika la Atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA limesema kuwa kamwe haiikubali hatua ya Iran ya kuendelea kuwazuia wawakilishi wa Shirika hilo kuzithibitisha hati za idara ya ujasusi zinazouelezea mpango huo.Kulingana na shirika la IAEA Iran ilifanya utafiti utakaoiwezesha kinyume na sheria kutengeza silaha ya nuklia.

Iran haitoi ushirikiano

Shirika hilo la IAEA limetoa picha kuwa Iran inakataa kuuelezea msimamo wake kuhusu kilichomo kwenye hati hizo na badala yake inajikita zaidi katika jinsi ya kuyawasilisha maelezo hayo.Mkurugenzi mkuu wa shirika la IAEA Mohamed El Baradei anaendelea kusisitiza kuwa IAEA inategemea ushirikiano wa mataifa husika ili kuzuwia usambaaji wa teknolojia ya nuklia,''Uwezo wetu wa kuifichua mipango ya nuklia ya siri unategemea uhuru tunaopewa na serikali husika ukizingatia misingi ya sheria.Sharti tuipe diplomasia kipa umbele pamoja na uchunguzi wa kina kufanywa hata kama itachukua muda mrefu. lazima mawasiliano yaendelee kati yetu na mataifa ambayo yanakabiliwa na utata kwasababu ya suala hili. Nguvu kamwe hazipaswi kutumiwa mpaka pale itakapohitajika.''alisisitiza

Ifahamike kuwa Iran imewasilisha ushahidi muhimu unaoashiria kuwa hati hizo si sahihi.Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Shirika la Atomiki lililo na makao yake mjini Vienna,Austria Ali Asghar Soltanieh aliwafahamisha baadhi ya maafisa wa IAEA kuwa hati hizo hazikuwa na alama zozote za kuisalama.

Muhuri rasmi

Mohamed El Baradei, Generaldirektor der Internationalen Atomenergiebehörde
Mkurugenzi mkuu wa IAEA anayeondoka Mohamed ElBaradei

Kwa ufupi hati zinazodaiwa kuwa zimetokea ngazi za juu za Wizara ya ulinzi hazikuwa na muhuri rasmi wa serikali ya Iran.Bwana Soltanieh aliyasema hayo alipozungumza na shirika la habari la IPS.Mwakilishi huyo wa Iran amesema kuwa amelitaja suala hilo mara kadhaa ila hakuna aliyemhoji kulihusu kila alipohudhuria vikao vya Bodi ya shirika la IAEA.

Shirika la Atomiki la IAEA kamwe halijawahi kukiri rasmi kuwa hati hizo hazikuwa na muhuri rasmi wa serikali ya Iran au alama zozote za kiusalama vilevile halijataja kuwa Iran imelalamika kuhusu suala hilo.Mwezi Mei mwaka 2008 ripoti ya shirika la IAEA ilieleza kuwa Iran ilisema kuwa hati hizo hazikuwa zimekamilika na kwamba muundo wake ulitofautiana.

Kinachoshangaza hapa ni kuwa bado haieleweki kwanini idara ya ujasusi ya Iran inaweza kuuondoa muhuri huo katika hati hizo muhimu jambo ambalo litazitia dosari.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya /AFPE-DPAE

Mhariri:Othman Miraji