1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi Zaendelea Kumtafuta Rais Mpya Ujerumani

19 Februari 2012

Mazungumzo ya awali kumtafuta rais mpya wa Ujerumani yanaendelea Jumapili, baada ya vyama vya kisiasa kushindwa kupata muafaka Jumamosi, siku moja baada ya Christian Wulff kujiuzulu kutokana na kuandamwa na kashfa.

https://p.dw.com/p/145W2
Christian Wulff baada ya kujiuzulu
Christian Wulff baada ya kujiuzuluPicha: picture-alliance/dpa

Kansela Angela Merkel ndiye anayeongoza mazungumzo hayo. Christian Wulff alijiuzulu Ijumaa baada ya Mwendeshamashtaka Mkuu kuomba kinga yake iondolewe, ili achunguzwe kwa kashfa zilizokuwa zikimkabili. Miongoni mwa kashfa hizo ni kupokea hisani ya kifedha kutoka kwa rafiki tajiri, na kutishia vyombo vya habari.   

Merkel ambaye alimteua bwana Wulff kuchukua wadhifa huo mwaka 2010 amekutana ofisini mwake na kiongozi wa chama cha Christian Social Union (CSU) Horst Seehofer, na Philipp Rösler wa chama cha Free Democratic, (FDP).

Kansela Angela Merkel anaongoza mazungumzo kumtafuta rais mpya
Kansela Angela Merkel anaongoza mazungumzo kumtafuta rais mpyaPicha: Reuters

Azma yake ni kufikia makubaliano na vyama hivyo washirika katika serikali, lakini pia ameshauriana na vyama vya upinzani vya Social Democrats (SPD), na Chama cha Kijani.

Baadhi ya majina yameanza kujitokeza

Miongoni mwa watu wanaopigiwa upatu kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Christian Wulff, ni Waziri wa Ulinzi Thomas de Maiziere, Waziri wa Mazingira Klaus Töpfer, Waziri wa Kazi Ursula von der Leyen, meya wa jiji la Frankfurt Petra Roth, na mwanasiasa kutoka Chama cha Kijani, Katrin Göring Eckardt. Sigmar Gabriel amempendekeza Joachim Gauck, mwanaharati siasa ya ukomunisti katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki kumrithi Wulff.

Kiongozi wa SPD Sigmar Gabriel na mwenzake wa Chama cha Kijani Jürgen Trittin wameweka masharti kwamba mtu atakayeteuliwa asiwe kutoka baraza la mawaziri, wala kigogo katika chama cha kisiasa.

Joachim Gauck, mmoja wa wanaopendekezwa kuwa rais mpya wa Ujerumani
Joachim Gauck, mmoja wa wanaopendekezwa kuwa rais mpya wa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Vyama vidogo vyataka kushirikishwa

Awali, akiongelea kushirikishwa kwa upinzani katika juhudi za kumtafuta rais mpya, Kansela Angela Merkel aliitaja tu SPD na Chama cha Kijani. Kiongozi wa Chama cha Mrengo wa Kushoto ambacho ni cha tatu kwa ukubwa katika kambi ya upinzani, Klaus Ernst, aliliambia gazeti la Rheinische Post kuwa lingekuwa jambo la busara kama Merkel angetafuta mawazo ya vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni.

Kiongozi mshirika wa Chama cha Kijani Cem Özdemir pia alimkosoa Kansela Merkel kukosa kukijumuisha Chama cha Mrengo wa Kushoto katika mazungumzo ya kumtafuta rais mpya, ingawa pia alikiponda chama hicho kukataa kumuunga mkono Gauck katika duru iliyopita.

Schloss Bellevue, Kasri ya Rais wa Ujerumani
Schloss Bellevue, Kasri ya Rais wa UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Ifikapo tarehe 18 Machi, Kongamano la Shirikisho linapaswa kuwa limemchagua rais mpya.

Wakati huo huo Mwendeshamashtaka Mkuu amekwishaanzisha uchunguzi juu ya shutuma kwamba rais aliyeondoka madarakani, Christian Wulff, alipokea fadhila kwa njia zisizo halali. Kashfa hiyo imekuwa ikimwandama Wulff tangu katikati mwa Desemba mwaka jana, hadi alipojiuzulu Ijumaa iliyopita.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpa/AP/AFP

Mhariri: Sudi Mnette