1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

240709 Reaktionen VW Porsche

Miraji Othman24 Julai 2009

Kampuni la magari la Porche linachanganyishwa na Volkswagen

https://p.dw.com/p/Iww4
Nembo za makampuni ya magari ya Kijerumani, Porsche na Volkswagen

Baada ya mkuu wa kampuni ya magari ya Porsche, Wendelin Wiedeking kujiuzulu wadhifa wake, sasa yamemalizika malumbano makubwa kabisa yasiokuwa na mfano ya kuwania madaraka katika historia ya uchumi wa hapa Ujerumani. Jambo moja ni wazi. Sasa makampuni ya magari ya Volkswagen na Porsche yataungana. Hata hivyo, kampuni la Porsche litabaki linajitegemea lenyewe. Hivyo ndivyo alivosisitita mshindi wa malumbano haya. Na wote walioshiriki katika malumbano haya yaonekana wamepumua na kutoshelezeka.


Baada ya kumalizika kupigana vikumbo na malumbano ya kuwania madaraka baina ya makampuni ya Porsche na Volkswagen, yaonesha watu wote wameridhika, hasa mshindi, yaani upande wa kampuni ya Volkswagen na pia waziri kiongozi wa mkoa wa Niedersachsen hapa Ujerumani, Christian Wulff:

" Suluhu hiyo ni nzuri kwa makampuni yote mawili, kwa wenye hisa wa kampuni zote mbili, pande zote mbili zinafaidika."

Pia mkuu wa Volkswagen, Martin Winterkorn, baada ya kikao cha bodi ya usimamizi ya kampuni yake, alifurahishwa na matokeo, na akasema:

"Tutasonga mbele pamoja na ujuzi wetu na pia kufanikiwa katika masoko ya dunia."

Pia upande wa kampuni la Porsche lililoshindwa katika malumbano haya unazungumzia kwamba suluhu hiyo ilikuwa nzuri. Mwenyewe mkuu wa zamani wa kampuni hiyo aliyelazimika kujiuzulu, Wendelin Wiedeking, alikuwa na matumaini, na alisema hivi saa chache baada ya kutangazwa kwamba amejiuzulu:

"Inavoonekana sasa ni kwamba kutakuwa na kampuni moja lililoungana, huo kwa hakika ulikuwa mkakati wetu, na huo ni uamuzi sawa."

Haijulikani kwa umbali gani Bwana Wiedeking alikuwa kweli anakusudia juu ya hayo aliyoyasema. Lakini yeye atalipwa uhondo wa marupurupu ya Euro milioni 50. Hata hivyo, mkuu huyo wa zamani wa kampuni la magari ya spoti la Porsche, lenye makao yake mjini Stuttgart, na aliyekuwa meneja mwenye kulipwa mshahara mkubwa kabisa hapa Ujerumani, anasifiwa sana na wafanya kazi wa kampuni hiyo. Hivyo, mkuu wa baraza la wafanya la kampuni hiyo, Uwe Hück, alitangaza kwamba meneja huyo atafanyiwa tafrija kubwa ya kuagwa, atapewa kwaheri isiokuwa ya kawaida.

Chini ya paa la Volkswagen, kwa vyovyote vile, kampuni ya Porsche itabakia na nembo yenye kujitegemea, kampuni hiyo ikiwa na makao yake makuu mjini Stuttgart. Na hivyo ndivyo, waziri kiongozi wa mkoa wa Niedersachsen, Christian Wulff, alivosisitiza tena:

"Tunajuwa kwamba nembo ya Porsche ni kitu kinachoenziwa, kwa hivyo tutailinda, tutailea, tutaiendeleza na tutaisaidia. Yote mengine na hayo yatakuwa sio mambo ya busara; na Porsche itabakia kuwa kampuni yenye kujitegemea yenyewe."

Hiyo ilikuwa risala muhimu kwa wafanyakazi alfu nane wa kampuni hiyo ya magari ya spoti, na ambayo imelemewa na deni la Euro bilioni kumi, hivyo kupigana hadi dakika ya mwisho ili liweze kunusurika.

Wafanya kazi waliohojiwa baada ya maafikiano hayo walisema wamefurahi kwamba watabakia na nafasi zao za kazi, na kwamba kampuni yao itaendelea kuweko. Wamepumua kwamba angalau sasa mambo yatakuwa tulivu.

Hadi katikati ya mwezi wa Agosti kutakuweko mauwafaka wa kimsingi. Hiyo ni pamoja na ufalme wa Qatar kuwa mwenye hisa ikitoa mtaji mpya wa Euro bilioni tano. Kwa hivyo sasa yamemalizika malumbano yaliokuwa hayana mfano katika historia ya uchumi wa Ujerumani, na pamoja imemalizika enzi ya Wendelin Wiedeking katika kampuni la Porche. Mwenyewe alisema hivi:

"Moyoni nauguwa, na kwa hivyo kwangu mimi ilikuwa wazi, lazima hapa tufikie mwisho, kwa bahti mbaya."

Mwandishi: Bauer, Knut

Mhariri: Josephat Charo