1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la dunia 2010.

18 Juni 2010

Serbia yaifunga Ujerumani 1-0.

https://p.dw.com/p/NwwQ
Mchezaji wa Serbia Milan Jovanovic, kushoto, akiifunga Ujerumani.Picha: AP

Bahati imeonekana kutoilalia timu ya taifa ya Ujerumani hii leo katika mpambano kati yao  na Serbia katika mchuano wa kundi D ya kombe la dunia baada ya kufungwa bao moja kwa sufuri na Serbia.

Serbia imeishangaza Ujerumani kwa bao lao moja baada ya Miroslav Klose kuondolewa uwanjani kwa kadi nyekundu  na Lukas Podolski  kukosa penalti katika mpambano huo.

Milan Jovanovic wa Serbia ndiye aliyefanikiwa kupachika wavuni goli hilo katika dakika ya 38,  muda mchache baada ya kupigwa fauli ya pili kwa Klose.

Ujerumani iliongoza mchezo kabla ya kuondoka kwa Klose, ikionyesha umahiri wake wa kulisakata kabumbu, hasaa katika masuala ya ushambulizi.

Süd Afrika WM 18.06.2010 Deutschland gegen Serbien
Miroslav Klose akionyeshwa kadi nyekundu na refa Alberto Undiano Mallenco.Picha: picture alliance/dpa

Mueller na Klose  kwa wakati wote walionekana kuwa tishio la timu hiyo ya Ujerumani, na munkari ulizidi kumpanda Klose pale goli alilolipachika  kunako nusu saa ya mchezo huo, kukataliwa kwa kusemekana alikuwa akiotea.

Mchezo uligeuzwa kichwa chini miguu juu dakika saba baadaye, wakati Klose alipopewa kadi hiyo nyekundu na kukifanya kikosi cha Ujerumani kusalia na wachezaji kumi dhidi ya 11 wa timu ya Serbia.

Kabla ya Wajerumani kumakinika kwa mshangao wa kuondolewa mchezaji wao, Serbia  ilipatiliza hali hii  na kutokana na ushirikiano mwema wa wachezaji wake, ilifanikiwa kufunga bao lao la ushindi  kupitia mchezaji wao nyota, Jovanovic.

Matokeo ya mchuano huu yanasemekana kuishusha hadhi timu hiyo ya Ujerumani ambayo iliwasili kwa michuano hiyo ya kombe la dunia  na imani ya ushindi hasa baada ya mchuano wao wa kwanza uliopelekea ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya Australia.

Hii pia inawapa matumaini timu ya Serbia  kufika rauni ya pili baada ya kufungwa na timu ya Afrika, Ghana bao 1-0.

Hata hivyo, Ujerumani bado inaongoza  katika kundi hilo D ikiwa na alama 3 kwa michuano miwili ambayo tayari imeshiriki  mbele ya timu za Ghana na Serbia ambazo pia zina alama 3 kila mmoja, huku ile ya Australia ikiwa haina alama zozote.

Australia inatarajiwa kupambana na Miamba ya Ghana siku ya Jumamosi, hapo kesho, katika uwanja wa Rustenburg na iwapo ushindi utawaangukiya, basi  nchi zote nne zitakuwa na pointi 3 kila mmoja, kuziwezesha kufuzu kwa awamu ya mwisho za michuano ya makundi wiki ijayo.

Mwandishi: Maryam Abdalla

Mpitiaji: Miraji  Othman