1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la G8 liongezwe?

Maja Dreyer4 Juni 2007

Nchi nane za kundi la G8 ni nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda, yaani Marekani, Canada, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Italy na Japan pamoja na Urusi ambayo iliingizwa miaka 9 iliyopita. Hata hivyo, kuna madai kwamba nchi nyingine ambazo zinaendelea haraka zinapaswa pia kuingizwa katika kundi hili. Nchi hizo ni China na India, na pia Brazil. Lakini je, nchi hizo kweli zina lengo la kuwa washirika wa kundi kubwa zaidi la G11?

https://p.dw.com/p/CHDE
Picha: AP

Kisiasa, dunia imegawanyika katika tabaka mbali mbali. Masuala ya kiuchumi yaliyo muhimu zaidi yanashughulikiwa na mataifa kadhaa muhimu ya kiuchumi. Pia, katika sera za usalama ni nchi chache tu zenye usemi, yaani nchi tano wanachama wa kudumu wa barala la usalama wa Umoja wa Mataifa zenye kura za turufu.

“Lakini ni wazi kwamba, katika siku za usoni lazima tuzishirikishe nchi kama China, India, Brazil na Misri, kwa sababu bila ya hizo hatutaweza kutatuta matatizo ya kimsingi." -Anayesema haya ni Georg Boogaarden, waziri mdogo wa nchi za nje wa Ujerumani. Kwa hivyo, licha ya nchi nane zilizostawi zaidi kiviwanda, mataifa mengine matano yanaalikwa kwenye mkutano wa G8 baadaye wiki hii kushiriki katika mazungumzo. Mataifa hayo ni China, India, Brazil, Mexiko na Afrika Kusini.

Kwengineko duniani, tayari China ina usemi mkubwa. Mfano ni barani Afrika ambapo China ni nchi muhimu ya kufanya biashara nayo sawa sawa na Marekani au nchi za Ulaya. Kwa hivyo, ni mara ya kwanza, nchi ambayo yenyewe ilikuwa nchi inayoendelea, na baado inapata msaada wa kimataifa na maeneo yake ni maskini, kuzisaidia nchi nyingine zinazoendelea. Katika nchi za Magharibi lakini kuna wasiwasi kwa sababu China inafanya biashara bila ya kujali kwa mfano haki za binadamu. India pia inazidi kupata umuhimu kiuchumi, hasa katika sekta ya kompyuta.

Ndio sababu, wanasiasa kadhaa walidai kundi la G8 liongezwe kuwa kundi la G11 au G13, kama alivyosema waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kabla ya mkutano uliopita. Lakini upinzani dhidi ya wazo hilo ndani ya G8 ni mkali.

Kwa upande mwingine, nchi husika pia hazipandishi sauti zao sana kuhusu suala la kuingizwa katika kundi la G8. Akiwa ni mgeni wa mkutano huu, lakini si mshirika, kiongozi wa China, Hu Jintao ana jukumu rahisi. Bado anaweza kuziwakilisha nchi zinazoendelea, kutoa miito au kuliunga mkono G8. Wakati huo huo anawez akuwaonyesha raia wake kuwa China ina umuhimu mkubwa duniani.

Brazil pia haipigania kuingia kwenye kundi la G8. Huyu hapa ni mshauri wa serikali ya Brazil, Paulo de Almeida: “Brasil ina hisia mbalimbali juu ya kupanda kwenye nafasi ya juu. Brazil inajiangalia kuwa kiongozi wa nchi zinazoendelea, pia tuna diplomasia kati ya nchi za Kusini. Iwapo tungekubali kuingizwa katika kundi kama la G11 au G8plus, basi Brazil itapoteza uaminifu wake kama kiongozi wa nchi zinazoendelea.”

Suala lingine ambalo haliwezi kujibiwa ni ikiwa kwa kulipanua kundi la G8, sera za kimataifa zitabadilika au zitabaki tu vilevile.