1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya kombe la Ulaya 2008

Ramadhan Ali30 Novemba 2007

Macho yanakodolewa jumapili hii Lucerne,Uswisi kwa kura ya jinsi timu 16 bora za Ulaya zitakavyoania konbe hilo.

https://p.dw.com/p/CV4T

Baada ya jumapili iliopita macho ya mashabiki wa dimba ulimwenguni yalikodolewa Durban,Afrika kusini kwa kura ya kombe la dunia 2010,kesho ni zamu ya mashabiki wa kombe la Ulaya la mataifa kutega sikio mjini LUCERNE,Uswisi.

Kura itapigwa huko kuamua vipi timu 16 bila ya Uingereza, zitaania kombe la Ulaya la mataifa juni,ijayo.Ligi maarufu za Ulaya, zinarudi nazo uwanjani na huko Namibia,wiki chache tu kabla kuanza Kombe la Afrika la mataifa nchini Ghana, kocha wake mzambia Ben Bamfuchile amejiuzulu-kisa nini ?

Euro-2008 –kombe la Ulaya la mataifa-la pili kwa ukali na msisimko duniani baada ya kombe la dunia la FIFA-litaanza Juni 7.Jumla ya miji 8 ya Uswisi na Austria zinazoandaa kwa ubia itachezewa mechi hizo:nayo ni Basle,Zurich,Berne na Geneva upande wa Uswisi.Nchini Austria ,dimba litasakatwa katika viwanja vya jiji kuu Vienna,ambako finali itachezwa Juni 29;Salzburg,Innsbruck na Klagenfurt.

Kura ya kesho huko Lucerne,inayopigwa wiki baada ya ile ya kombe la dunia huko Durban,Afrika Kusini inafanyika chini ya biramu: “Tarajia msisimko” na kombe la Ulaya daima limejaa msisimko.

Wagiriki waliozusha msisimko huo mara iliopita chini ya kocha mjerumani Otto Rehagel, wamehakikisha tayari watatetea taji lao Juni mwakani.Kwani, walishinda mechi 10 kati ya 12 za kuania tiketi za Uswisi na Austria.Timu nyengine zinazosubiri kwa shauku kuu kura ya kesho ni mabingwa wa dunia-Itali,mabingwa mara 2 wa Ulaya-Ufaransa na washindi mara 3 –Ujerumani.

Kiasi cha tiketi milioni 1 zitauzwa kwa changamoto hizo za wiki 3 zitakazotanguliwa na Kombe la afrika la mataifa nchini Ghana,Januari hii.

Namibia ni miongoni mwa timu 16 za Afrika zilizokata tiketi za kwenda Ghana-hii ikiwa ni mara ya pili kwa namibia kufanya hivyo.

Kwa msangao wa mashabiki wengi, kocha wao –mzambia Ben Bamfuchile ametangaza kujiuzulu.

Bamfuchile alishangiriwa na kubebwa kiti-kiti kama shujaa hapo Septemba mwaka huu, baada ya Namibia kuizaba Ethiopia 3-2 na kutoroka na tiketi ya Accra ikwaacha nyuma simba wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na hata Libya.

Namibia ina miadi na Senegal,Januari 13 kupimana nguvu kabla ya timu zote 2 kuania kombe hilo.

Ligi maarufu za Ulaya-Bundesliga-Premier League,Serie A na La Liga-zinarudi uwanjani mwishoni mwa wiki hii tena kwa kishindo:

Bayern Munich,itasamehewa mara hii kwa kutumai Werder Bremen na Hamburg-mahasimu wake 2 wakubwa wanaoifukuzia kileleni wanatoka sare kila moja ikipoteza pointi 2.Kwani, Bremen iliotamba majuzi ilipoizaba Real Madrud 3-2 katika champions League na Hamburg,iliokata tiketi yake ya duru ijayo ya kombe la ulaya la UEFA,msimu huu zinatamba kweli.

Munich imetambua hayo,kwani ushindi leo wa ama Bremen au Hamburg, utaiweka moja ya timu hizo kileleni mwa Ligi.

B.Munich ilikosa juzi nafasi ya kujiunga na Hamburg katika duru ijayo ya kombe la UEFA kwa kumudu suluhu tu na Braga.

Mabingwa Stuttgart wana miadi na Borussia Dortmund wakati mpambano mwengine wa kusisimua ni kati ya Berlin na Leverkusen.

Ama vilio kuwa Martin O’Neill awe kocha mpya wa Uingereza, vitazdi kuhanikiza ikiwa Aston villa itakomesha leo rekodi ya Arsenal kutamba tangu kuanza msimu huu.Villa imekua nayo ikishinda karibuni na ingawa O’Neill hana tamaa kubwa ya ukocha wa England,ushindi leo,utakuza nafasi zake.Chelsea ina miadi leo na West Ham United wakati Wigan Athletic wanaonana na Manchester city.

Katika La Liga-Ligi ya Spain, Real Madrid inachuana na Racing Santander wakati FC Barcelona, wanapambana na Espanyol.

Kwenye Ligi ya Itali,mabingwa wa Ulaya AC Milan, wana miadi na mahasimu wao Juventus.