1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon yatumbukia katika mzozo mkubwa wa kisiasa

24 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CSgt

Lebanon imeachwa bila kiongozi hii leo baada ya rais Emile Lahoud kuondoka madarakani kufuatia muhula wake kumalizika bila bunge kumchagua rais mpya.

Hatua ya rais Lahoud imesababisha mpasuko mkubwa wa ksiasa nchini Lebanon. Kiongozi huyo ameondoka ikulu ya rais mjini Beirut muda mfupi kabla saa sita usiku wa kuamkia leo na kukabidhi usalama wa nchi kwa jeshi la Lebanon.

Akizungumza muda mfupi kabla kuondoka ikulu kwenda katika nyumba yake binafsi iliyo karibu, rais Lahoud amesema dhamiri yake ni safi na Lebanon iko salama. Ameongeza kuwa ipo haja ya Walebanon kumchagua rais mpya haraka kwa sababu baraza la mawaziri linaloungwa mkono na Marekani na Ulaya si halali. Emile Lahoud ameonya ikiwa hilo halitafanyika Lebanon italipa gharama kubwa.

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Lebanon, Walid Jumblatt, amesema imekuwa kazi kubwa kumuondoa madarakani rais Emile Lahoud. ´Lakini sasa ameondoka na haijulikani kitakachotokea. Ametoa mwitho ari ya amani na uthabiti iheshimiwe.´

Baraza la mawaziri linaloongozwa na waziri mkuu Fouad Siniora limesema limechukua madaraka ya kuitawala nchi mpaka bunge litakapokubaliana kuhusu atakayekuwa rais mpya.

Timor Gocksel wa chuo kikuu cha Marekani mjini Beirut amesema suluhisho pekee ni wadhamini nje ya Lebanon wakubaliane.

Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za kiarabu, kama vile Saudi Arabia, Misri na Jordan, zinatarajiwa kuyatambua madaraka ya baraza la mawaziri.

Lakini muungano wa upinzani unaoongozwa na kundi la kishia la Hezbollah, linaloungwa mkono na Syria na Iran, umesema Lebanon haina rais.