1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen yatupwa nje ya kombe la ligi Ulaya

Aboubakary Jumaa Liongo18 Machi 2011

Bayer Levekusen,walisukumizwa nje ya michuano hiyo, baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Villarreal ya Uhispania.Levekusen imesukumizwa nje kwa jumla ya mabao 5-3.

https://p.dw.com/p/10bnS
Mshambuliaji wa Villarreal Borja Valero(katikati) akikokota mpira, mbele ya beki wa Leverkusen Sami Hyypia.Picha: dapd

Kutolewa kwa Leverkusen ambayo inakamata nafasi ya pili katika ligi ya Ujerumani Bundesliga,kumeifanya Ujerumani kubakia na timu moja tu katika michuano ya Ulaya, ambayo ni Schalke 04 iliyofuzu kwa robofainali ya ligi ya mabingwa.

Wakati watengeneza dawa hao kutoka mji wa Leverkusen wakipewa mkono wa buriani katika michuano hiyo, timu mbili za Uingereza, Liverpool na Manchester United, nazo zimepigwa kumbo.

Liverpool ililazimishwa nyumbani kutoka suluhu bin suluhu na Braga ya Ureno, ambayo katika mechi ya kwanza ilishinda bao 1-0.Timu hiyo ya Ureno haijawahi kushinda hata ubingwa wa ligi huko Ureno, lakini ilionesha ushupavu wa hali ya juu kulinda bao lake na hivyo kuwasukumiza nje Liverpool.

Manchester City ikicheza nyumbani mjini Manchester iliichapa Dynamo Kiev bao 1-0, bao ambalo hata hivyo halikutosha kuwafanya wasonge mbele, kwani katika mechi ya kwanza walichapwa mabao 2-0.

City ilishuhudia mshambuliaji wake Mario Balotelli akipewa kadi nyekundu katika dakika 36 ya mchezo.Kocha wa timu hiyo Roberto Mancini alielezea kusikitishwa kwake na kupigwa huko kumbo , pamoja na kwamba kikosi chake kilikuwa na wachezaji wengi mahiri.

Ureno ilishuhudia timu zake zote tatu zikifuzu kwa robofainali, ambapo mbali ya Braga iliyoisukumiza nje Liverpool,Benfica na FC Porto, nazo pia zilikata tiketi yake kwa hatua hiyo.Benfica ikicheza ugenini mjini Paris ililazimisha sare ya bao 1-1 kwa wenyeji wao Paris St Germain na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2.

Nayo Porto ilitumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwa kuchapa CSKA Moscow ya Urusi mabao 2-1 na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-1.

Uholanzi ilishuhudia timu zake mbili zikifuzu, huku wakongwe wao Ajax Amsterdam wakifurushwa nje ya michuano hiyo na Spartak Moscow ya Urusi kwa jumla ya mabao 4-0.Ajax hiyo jana ilikandikwa mjini Moscow mabao 3-0.

Lakini Twente Enschede na PSV Eindhoven ziliwafuta machozi washabiki wa Uholanzi pale zilipofuzu.Enschede pamoja na kuchapwa ugenini mabao 2-0 na Zenit St Petersburg ya Urusi lakini imeweza kusonga mbele kufuatia ushindi wake wa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza.Nayo Eindhoven iliichapa Rangers ya Scotland bao 1-0 tena ugenini na hivyo kufuzu kwa robofainali.

Wakati huo huo, ratiba ya robofainali ya ligi ya mabingwa inatarajiwa kupangwa leo hii mchana huko Lyon Ufaransa.

Uingereza imeingiza timu tatu katika hatua hiyo ya robofainali ambazo ni Manchester United,Chelsea na Tottenham Hotspur, huku Uhispania ikiwa na timu mbili, Barcelona na Real Madrid,Ujerumani bendera yake inapeperushwa na Schalke 04, huku mabingwa watetezi Inter Milan ya Italia na Shakhtar Donetsk ya Ukarine zinakamilisha timu hizo nane.

Kati ya timu hizo, Barcelona ndiyo inayopigiwa upatu mwaka huu kutoroka na kombe, na hakuna timu ambayo ingependa kukutana nayo katika ratiba hiyo.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters

Mhariri:Hamidou Oummilkheir