1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Polisi yazima shambulio la magaidi

29 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBnF

Polisi imegunduwa shambulio la kigaidi leo hii karibu na mtaa wa Piccadily Circus mjini London kwa kuteguwa mripuko wa bomu kwenye gari lililokuwa limesheheni mafuta,mitungi ya gesi na misumari baada ya wafanyakazi wa gari la wagonjwa kuona moshi ukitokea kwenye gari hilo aina ya Mercedes lililokuwa limeegeshwa.

Polisi imesema katika taarifa kwamba wataalamu wa mabomu waliitwa kuchunguza gari hilo lililoegeshwa kwenye Haymarket mtaa wenye harakati kubwa katikati ya eneo lenye majengo mengi ya kumbi za sinema na michezo ya kuigiza mapema leo asubuhi.

Maafisa wa kupambana na ugaidi wanaendelea na uchunguzi kwenye mtaa huo ambao umefungwa na yumkini ukaendelea kufungwa kwa muda mkubwa ujao.Mkuu wa polisi ya kupiga vita ugaidi nchini Uingereza Pater Clarke amesema miripuko ya bomu hilo ilikuwa na nguvu kubwa kuweza kusababisha majeraha na vifo.

Wakati waziri wa mambo ya ndani Jacqui Smith akiiitisha mkutano wa dharura wa maafisa waandamizi Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ametowa wito kwa wananchi wa Uingereza kuendelea kuwa macho.

Hapo tarehe saba mwezi wa Julai miaka miwili iliopita abiria 52 waliuwawa na mabomu yaliotegwa na magaidi kwenye treni na basi mjini London.