1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Tajiri wa Urusi ataka Putin apinduliwe

13 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCAE

Tajiri mkubwa wa Urusi anayeishi uhamishoni Boris Berezovsky hapo jana ametowa wito wa kupinduliwa kwa kutumia nguvu Rais Vladimir Putin wa Urusi na kutishia kuzidi kudhoofisha uhusiano kati ya serikali ya Uingereza na Urusi.

Serikali ya Uingereza ambayo uhusiano wake na Urusi umeathirika vibaya kutokana na mauaji ya mpelelezi wa zamani wa Urusi Alexander Litvinenko mara moja imejitenganisha na matamshi hayo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje amesema wanalaani wito wowote ule kwa kupinduliwa kwa kutumia nguvu taifa lililo huru na kwamba wanategemea kila mtu anayeishi au kufanya kazi nchini Uingereza au kuitembelea nchi hiyo bila ya kujali hadhi yao watafuata sheria za nchi.

Tajiri huyo wa Urusi anayeishi Uingereza ambaye aliikimbia nchi yake hapo mwaka 2000 ameliambia gazeti la the Guardian kwamba utawala wa sasa katika Ikulu ya Urusi hauwezi kuondolewa kwa njia za kidemokrasia na kwamba hakuna chaguo jengine isipokuwa kutumia nguvu.

Hususan amesema kwamba amekuwa na mawasiliano na watu fulani wenye ushawishi mkubwa nchini Urusi na kwamba amekuwa akihusika katika kuugharimia mpango huo.