1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya The Hague kutomshtaki kiongozi wa waasi wa Darfur

9 Februari 2010

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya The Hague, Uholanzi imesema kuwa haitoweza kumfungulia mashtaka kiongozi wa waasi wa Darfur Bahar Idriss Abu Garda kuhusiana na mauaji ya wanajeshi 12 wa Umoja wa Afrika mwaka 2007

https://p.dw.com/p/Lwoc

Mahakama hiyo imesema hakuna ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka kiongozi huyo.

Hukumu hiyo imetoka mnamo wakati ambapo Rais Idriss Derby wa Chard akiendelea na ziara yake nchini Sudan katika juhudi za kuimarisha uhusiano kati ya pande hizo mbili,Huku Kamati maalum ya kutafuta suluhisho ya mzozo wa Sudan ya Umoja wa Afrika inayoongozwa na Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki ikiwa nchini Kenya.

Katika hukumu yake , mahakama hiyo ya The Hague imesema kuwa, haijaridhishwa na ushahidi uliyowasilishwa kutaka kiongozi wa waasi wa Darfur afunguliwe mashtaka.

Waendesha mashtaka wa mahakama hiyo walitaka kufunguliwa mashtaka kwa kiongozi huyo Idriss Abu Garda, akituhumiwa kwa makosa matatu ya uhalifu wa kivita, yakiwemo mauaji na utekaji nyara.

Wanataka Abu ashtakiwe kutokana na wapiganaji wake kuwaua wanajeshi 12 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika, kabla ya kufanya uporaji katika kambi yao kaskazini mwa Darfur Septemba 29 mwaka 2007.

Wengi wa askari hao wa Umoja wa Afrika waliyouawa walitoka, Botswana,Gambia, Nigeria, Mali na Senegal.Waendesha mashtaka hao wamesema kuwa wanatarajia kukata rufaa kupinga hukumu hiyo, na kwamba wanaamini wana ushahidi wa kutosha kumtia hatiani kiongozi wa waasi wa Darfur.

Wakili wa Abu Garda,Karim Khan ameupongeza uamuzi wa mahakama hiyo ya The Hague akisema kuwa mteja wake ana imani na uhuru pamoja na subira ya mahakama hiyo, katika kutoa maamuzi.

Ikumbukwe ya kwamba Mahakama hiyo hiyo ya The Hague imekwishatoa waranti wa kukamatwa kwa Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan ikimtuhumu kuhusika kwake na mauaji ya halaiki ya Darfur.

Wiki iliyopita kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo ya The Hague kiliielekeza mahakama hiyo kufikiria upya uamuzi wake na kutojumuisha mashtaka ya uhalifu wa mauaji ya halaiki katika waranti wa kukamatwa Rais Bashir.Umoja wa Afrika ulitangaza kutokubaliana na waranti huo

Mjini Nairobi Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki ambaye anaongoza ujumbe wa kamati maalum ya Umoja wa Afrika, kutatua mzozo wa Sudan akiwemo pia rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya, amesema kuwa moja ya mapendekezo ya kamati yake ni suala la Sudan kushughulikiwa na mahakama ya Sudan

Sudan Präsident Omar el-Bashir Idris Deby
Rais Omar el-Bashir wa Sudan kulia akimpokea Rais wa Chad Idris Deby mjini KhartoumPicha: AP

´´Kama mahakama ya taifa inaweza kushughulikia masuala hayo, basi iache ishughulikie.Na ni lazima ianzishwe kikatiba mahakama yenye nguvu, hayo ni baadhi ya mapendekezo, mahakama ambayo itaundwa na majaji wa Sudan ambao wataungana na majaji watakaoteuliwa na Umoja wa Afrika ´´

Ujumbe huo uko mjini Nairobi ambako leo unatarajiwa kukutana na Rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi.Kenya ndiyo iliyokuwa mwenyeji wa mazungumzo yalipelekea kufikiwa kwa mkataba wa amani na kumaliza miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Sudan Kaskazini na Kusini.

Katika hatua nyingine Rais Idriss Derby wa Chad anaendelea na ziara yake nchini Sudan, ziara ambayo mjumbe wa Marekani katika mzozo wa Darfur Scott Gration ameilezea huenda ikarejesha amani na usalama katika eneo la Darfur.

Chad na Sudan zimekuwa katika uhusiano zikituhumiana kwa kuwasaidia waasi wa pande zote mbili.Mwezi uliyopita zilikubaliana kuweka majeshi ya pamoja katika mpaka wake katika kurejesha hali ya usalama.

Akizungumza kwa njia simu na shirika la habari la Ufaransa AFP kutokea Washington,mjumbe huyo wa Marekani Scott Gration amesema kuwa wamefurahishwa sana na hatua ya serikali zote mbili kunyoosheana mkono wa urafiki.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/AFP/Kiti´s oton

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman