1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala wa bunge kuhusu jukumu la jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan

Oumilkher Hamidou26 Novemba 2009

Kadhia ya kuripuliwa malori yaliyotekwa nyara Kundus na kugharimu maisha ya watu 140,yamgharimu wadhifa wake mkuu wa vikosi vya Ujerumani na katibu wa dola mmoja

https://p.dw.com/p/Kh6r
Waziri wa zamani na mpya wa ulinzi (kutoka kulia)Jung na zu GuttenbergPicha: AP

Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani,zu Guttenberg amewaachisha kazi hii leo ,mkuu wa vikosi vya wanajeshi na katibu wa dola katika wizara ya ulinzi.Habari hizo zimetangazwa na waziri zu Guttenberg bungeni hii leo.Sababu aliyotoa mwanasiasa huyo wa kutoka chama cha CSU ni ile hali ya kuficha ripoti kuhusu kuhujumiwa kwa mabomu malori mawili yaliyosheheni mafuta,yaliyokua yametekwa nyara na wataliban,mapema mwezi September mwaka huu nchini Afghanistan.Shambulio hilo limegharimu maisha ya raia kadhaa.

Kimsingi bunge lilikua lijadiliane kuhusu mpango wa kurefushwa muda wa shughuli za vikosi vya Ujerumani-Bundeswehr nchini Afghanistan.Badala yake lakini mjadala huo ukachukua sura ya malumbano makali kuhusu mchango wa waziri wa zamani wa ulinzi Franz-Josef Jung.Mwanasiasa huyo wa chama cha CDU,kwa mujibu wa vyombo vya habari,ameficha habari kuhusu shambulio hilo la madege ya kivita ya jeshi la shirikisho-Bundeswehr,mwezi September uliopita nchini Afghanistan.Katika shambulio ,hilo dhidi ya malori yaliyosheheni mafuta yaliyotekwa nyara na wataliban,karibu na Kundus,kaskazini mwa Afghanistan,watu wasiopungua 140 wanasemekana wameuwawa,na wengi kati yao ni raia wa kawaida.Gazeti la Die Bild Zeitung limeandika katika toleo lake la leo kwamba ripoti ya polisi ya kijeshi kuhusu kadhia hiyo imefichwa,hakuna aliyekua akiijua,si jamii na wala si mwanasheria mkuu.

Akihutubia bungeni hii leo aliyeshika nafasi ya Franz-Josef Jung,Karl-Theodor zu Guttenberg ametangaza hatua za mwanzo kuhusu kadhia hiyo:

"Mkuu wa vikosi vya wanajeshi,ameniomba nimvuwe jukumu lake,sawa na katibu wa dola Wichert aliyejibebesha dhamana.Hata kama mtacheka,nnaitumia fursa hii kuwashukuru kwa mchango wao."

Franz Josef Jung Wolfgang Schneiderhan
(kushoto) mkuu wa vikosi vya wanajeshi Wolfgang Schneiderhan pamoja na waziri wa zamani wa ulinzi JungPicha: AP

Hata hivyo upande wa upinzani haujaridhika na hayo.Mwanasiasa wa kutoka chama cha walinzi wa mazingira Hans Christian Ströbele amemtaka zu Guttenberg arekebishe matamshi yake,alipokadiria kwamba shambulio hilo lilikua la lazma.Nae mbunge wa kutoka chama cha SPD Johannes Flug akasisitiza juu ya haja ya kuundwa tume ya uchunguzi.

Mbunge wa chama cha mrengo wa kushoto-Die Linke amekwenda umbali wa kudai waziri wa zamani wa ulinzi,ambae ni waziri wa ajira katika serikali mpya ya nyeusi na manjano, Franz-Josef Jung ,ajiuzulu.

Jaribio la upande wa upinzani la kutaka kumlazimisha Franz-Josef Jung ajieleze bungeni,limeshindwa kutokana na wezani wa nguvu kati ya na vyama vinavyounda serikali mpya ya muungano vya CDU/CSU na waliberali wa FDP.Hata hivyo waziri Jung ameahidi kujibu dhana hizo.Kabla ya hapo lakini anasema anataka kuzisoma kwa makini ripoti za vyombo vya habari.

Hata kabla ya amjadala wa bunge,waziri huyo wa zamani wa ulinzi alizisuta ripoti kwamba ameficha habari kuhusu mashambulio ya Kundus.

Majadiliano makali kuhusu sera za habari za wizara ya ulinzi yamegubika mjadala wa bunge kuhusu kurefushwa muda wa shughuli za wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan.Hata hivyo dalili zimechomoza kwamba wingi wa wabunge wataunga mkono kurefushiwa muda wanajeshi hao, mpango huo utakapojadiliwa tena wiki ijayo.

Mwandishi:Bettina Marx (DW Berlin)/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Aboubakary Liongo

: