1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco yajikatia tikiti ya Urusi 2018

Bruce Amani
13 Novemba 2017

Morocco siku ya Jumamosi ilifuzu kwa mara ya tano baada ya kuilaza Cote d'Ivoire mabao mawili kwa bila. Ushindi huo ulisababisha vurugu mjini Brussels

https://p.dw.com/p/2nX5z
Fußball WM Playoffs | Elfenbeinküste vs. Marokko
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Polisi 20 walijeruhiwa, maduka yakaporwa na magari kuchomwa moto. Tunisia na Nigeria ni mataifa mengine ya Afrika ambayo yatatamba Urusi mwaka ujao.

Misri ambao tayari wana tikiti ya Kombe la Dunia, walimaliza kampeni yao ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka wa 2018 kwa kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Ghana. Congo ilitoka sare ya 1-1 na Uganda.

Michuano ya kufuzu ya barani Afrika itakamilika leo ambapo senegal ambao tayari wanaelekea Urusi watawaalika Afrika Kusini na Burkina Faso watakutana na Cape Verde.

Fußball WM Playoffs | Elfenbeinküste vs. Marokko
Mashabiki wa Morocco walisababisha vurugu BrusselsPicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

CHAN

Tuelekee Afrika Mashariki ambapo Rwanda jana ilinyakua tikiti ya mwisho ya kushiriki fainali za dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani mwaka wa 2018 maarufu kama CHAN, licha ya kutoka sare tasa na Ethiopia mjini Kigali katika mchuano wa mkondo wa pili wa mechi ya mchujo.

Wanyarwanda walifuzu kwa jumla ya mabao matatu kwa mawili baada ya kushinda mechi ya mkondo wa kwanza kwa mabao hayo mjini Addis Ababa wikiendi iliyopita.

Misri ilijiondoa kutoka kinyang'anyiro hicho ikitaja sababu ya vilabu kukataa kuwaruhusu wachezaji wao kwenda kuichezea timu ya taifa, na hilo likaipa Rwanda na Ethiopia fursa ya pili ya kufuzu. Nchi zote mbili lishindwa katika hatua ya mwisho ambapo Rwanda iliangushwa na Uganda wakati Ethiopia ikibwagwa na Sudan. Kenya walipokonywa kibali cha kuwa wenyeji wa dimba hilo linaloandaliwa kila baada ya miaka miwili baada ya kuchelewesha matayarisho ya dimba hilo na Morocco ikaipiku Guinea ya Ikweta katika harakati za kupewa haki ya kuchukua nafasi ya Kenya. Droo ya dimba hilo la nchi 16 irafanywa mjini Rabat Ijumaa hii ambapo dimba hilo litaanza kutifua vumbi Januari 12 hadi Februari 4 katika miji ya Agadir, Casablanca, Marrakech na Tangier.

Angola, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Guinea ya Ikweta, Guinea, Ivory Coast, Libya, Mauritania, Namibia, Nigeria, Sudan, Uganda na Zambia zinakamilisha orodha hiyo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Moahammed Abdul-Rahman