1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOSCOW: Urusi yamtambua Abbas kama kiongozi wa Wapalestina

30 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBdg

Urusi imesema leo inamtambua rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, kama kiongozi wa Wapalestina wote.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, amemwambia rais Abbas kwamba Urusi inaziunga mkono juhudi za amani za kutafuta suluhisho la mzozo unaoendelea katika maeneo ya Wapalestina.

Rais Abbas yumo nchini Urusi kwa ziara rasmi ya siku tatu na amepangiwa kukutana na rais wa Urusi, Vladamir Putin, wakati wa ziara yake hiyo kuzungumzia matatizo yanayoendelea katika maeneo ya Wapalestina.

Abbas aliwasili jana mjini Moscow katika ziara ya kwanza tangu kundi la Hamas lilipolidhibiti eneo la Ukanda wa Gaza mnamo mwezi Juni mwaka huu na anatazamia kumshawishi rais Putin amuunge mkono pamoja na chama chake cha Fatah.

Rais Abbas amesema urafiki baina ya Urusi na Palestina ni wa kihistoria na Wapalestina wataendelea kuulinda na kuuimarisha.

Urusi ni mwanamchama wa pande nne zinazoudhamini mpango wa amani ya Mashariki ya Kati zikiwemo pia Marekani, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.