1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Paul Krugman apewa tuzo la Nobel la Uchumi -2008

Kalyango Siraj13 Oktoba 2008

Ni mkosoaji wa utawala wa Bush

https://p.dw.com/p/FYbN
Paul KrugmanPicha: picture-alliance/ dpa

Tuzo la Nobel la masuala ya kiuchumi la mwaka huu limemwendea raia wa Marekani Paul Krugman, ambae ni mkosoaji mkuu wa rais Bush.Tuzo hilo linaombatana na pesa taslim Euro millioin moja atalipokea rasmi mwezi Disemba.

Taasisi ya kiakademia kuhusu masuala ya sayansi ya Sweden,The Royal Swedish Academy of Science, imetangaza mshindi wa mwaka huu wa tuzo hilo kutokana na nadharia yake mpya inayotathmini athari za masoko huria pamoja na utanda wazi.Pia nadharia hiyo inachunguza sababu ambazo zinachangia ukuaji wa miji duniani.

Taasisi ya sayansi katika taarifa yake imeeleza kuwa nadharia ya Krugman inaegemea kigezo kuwa bidhaaa na huduma vinaweza kuzalishwa kwa wingi tena bila gharama kubwa katika walichokiita mlolongo mrefu.Nadharia hii imekuwa ikijulikana, katika lugha ya kiuchumi kama, wekevu wa mizani yaani kupungua kwa gharama za wastani za zao la baada ya uzalishaji wa muda mrefu wa zao hilo kutokana na upanuzi wa kiwango cha mazao yanayopatikana.

Nadharia hii ya Krugman inafafanua kwanini biashara imetawaliwa na nchi ambazo sio tu zina hali zinazofanana lakini pia hushirikiana kibiashara katika bidhaa zinazofanana.

Kamati hiyo iliamua Sweden kama mfano huo kwani sio tu inauza nje magari lakini pia inayaagiza kutoka ng'ambo.

Kutokana na hayo ndio sababu taasisi hiyo ikamumchagua Paul Krugman kama mshindi wa mwaka huu wa tuzo hilo.

Krugman,alizaliwa Febuari 28 mwaka wa 1953 katika jimbo la New York la Marekani.

Ana shahada ya tatu ya digrii yaani PhD na ni mwalimu wa uchumi na masuala ya kimataifa katika chuo kikuu cha Princeton New Jersey nchini Marekani.

Pia amewahi kufundisha katika vyuo mbalimbali kama vile Chuo kikuu cha Yale,Chuo cha Uchumi cha London School of Economics, pamoja na Stanford.

Ameandika vitabu mbalimbali kuhusu masuala ya uchumi.Isitoshe huandika makala yanayotoka mara mbili kwa wiki katika gazeti la The New York Times. Katika makala hayo mara kadhaa anazichamba sera za kigeni pamoja na za mambo ya ndani za rais Bush.

Amewahi kutumikia baraza la Marekani la washauri wa masuala ya kiuchumi.Pia aliwahi kupewa medali ya John Bakes Clark ya mwaka wa 1991. Medali hiyo ni tuzo linalotolewa kila baada ya miaka miwili na chama cha Marekani kinachohusika na masula ya kiuchumi, kwa mwanauchumi ambae ana umri uliochini ya miaka 40.

Kwa leo Krugman ana umri wa miaka 55.Tuzo la mwaka huu,likiambatana na donge la takriban Euro millioni moja, atalipokea rasmi katika sherehe maalum itakayofanyika tarehe 10 Disemba mjini Stockholm nchini Sweden.