1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa benki ya dunia akabiliwa na tuhuma kadha.

Sekione Kitojo14 Aprili 2007

Katika nafasi tano za juu za ajira kimataifa zilizofanywa na rais wa benki ya dunia anayekabiliwa na tuhuma Paul Wolfowitz katika kipindi chake cha utawala cha miaka miwili , tatu zilikuwa za wanasiasa waandamizi wa serikali za mrengo wa kulia ambazo zilikuwa waungaji mkono wakubwa wa sera za Marekani nchini Iraq. Ajira ya mwisho ilifanyika mwezi uliopita wakati naibu wa zamani wa waziri mkuu Marwan Muasher alipoteuliwa kuwa makamu wa rais kwa ajili ya masuala ya kigeni.

https://p.dw.com/p/CHGH
Paul Wolfowitz rais wa benki ya dunia: Mdomo wazi baada ya kuandamwa na tuhuma kadha.
Paul Wolfowitz rais wa benki ya dunia: Mdomo wazi baada ya kuandamwa na tuhuma kadha.Picha: picture-alliance/dpa

Muasher alitumikia katika wadhifa wa balozi wa Jordan mjini Washington wakati wa kuelekea vita vya Iraq mwaka 2002 na anaripotiwa kuwa alichukua jukumu muhimu katika kuhakikisha kuwa ushirikiano wa Jordan katika uvamizi wa Iraq March mwaka 2003.

Wakati na baada ya uvamizi huo, wakati akiwa kama waziri wa mambo ya kigeni na baadaye kama naibu waziri mkuu, alikuwa akionekana miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa Marekani katika ulimwengu wa Kiarabu ambao ulikuwa ukizidi kuleta upinzani.

Kuteuliwa kwa Muasher kunakuja miezi tisa baada ya Wolfowitz kumteua waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Hispania Ana palacio kuwa makamu wa rais mwandamizi na mshauri mkuu.

Akiwa kama waziri wa mambo ya kigeni , alikuwa muungaji mkono wa wazi wa uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq, ambapo serikali yake, wakati huo ikiongozwa na waziri mkuu wa zamani Jose Maria Aznar, ilichangia wanajeshi 1,500 kwenda Iraq.

Pia mwezi Juni 2006, Wolfowitz alimteua waziri wa zamani wa fedha wa Salvador Juan Jose Daboub kuwa mmoja kati ya wakurugenzi watendaji wawili wa benki hiyo. Kwa nyongeza katika wadhifa wake wa fedha , Daboub ametumikia kama mkuu wa utawala katika serikali ya zamani ya rais Francisco Flores, wakati ikiwa kama mwanachama wa majeshi ya muungano yaliyoongozwa na Marekani , alituma wanajeshi 400 wa Salvador nchini Iraq, zaidi kuliko nchi yoyote inayoendelea.

Wolfowitz hivi sasa anakabiliana na miito ya kujiuzulu, hususan kutoka kwa wafanyakazi wa benki hiyo, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na idadi kadha ya maafisa waandamizi wa zamani wa benki hiyo, ili ajiuzulu kuhusiana na madai kuwa amejihusisha kinyume na utaratibu kumpandisha cheo pamoja na kumpa marupuru ya ziada mpenzi wake wa kike, Shaha Riza, mfanyakazi wa benki na mtaalamu wa mambo ya benki ambaye amepelekwa katika wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani.

Wolfowitz ambaye amekuwa rais wa benki kuu ya dunia Juni 2005, amekuwa akisisitiza kuwa jukumu lake kama naibu waziri wa ulinzi wa Marekani chini ya utawala wa rais George W. Bush , ambapo alikuwa msanifu muhimu katika vita vya Iraq, hautaweza kuwa na athari katika maamuzi yake katika benki hiyo.

Lakini juhudi za Wolfowitz kumteua meneja mpya wa benki hiyo nchini Iraq licha ya wasi wasi kuhusu hali ya usalama nchini humo, pamoja na juhudi za benki hiyo za kuzuwia ripoti juu ya tukio ambapo mfanyakazi wa benki hiyo alijeruhiwa mjini Baghdad, ili kuweza kuzuwia juhudi hizo za kumteua meneja huyo, zimetoa ushahidi kwa wakosoaji kuwa amekuwa akiiweka taasisi hiyo na mali zake karibu na sera za Marekani.

Ukweli kwamba Wolfowitz pia aliwachukua wasaidizi muhimu wa mrengo wa kulia kufanyakazi katika benki hiyo, ambapo hakuna hata mmoja mwenye ujuzi katika masuala ya maendeleo, ambao walifanyakazi kwa karibu nae kuhusiana na suala la Iraq wakati akiwa katika wizara ya ulinzi pia inaongeza nguvu muonekano huo.

Naamini kuwa Paul Wolfowitz ametumia muda wake madarakani kwa kiasi kuzizawadia serikali na watu binafsi ambao waliisaidia sana serikali ya Marekani katika vita vyake na Iraq, amesema Steven Clemens, mkurugenzi wa mpango wa mikakati ya Marekani katika wakfu wa Marekani, ambaye amekuwa akifuatilia kwa karibu kazi ya Wolfowitz katika tovuti ya Blog ya kiongozi huyo. Kwangu mimi hii ni hatua ya utovu wa uwezo katika kuiongoza taasisi muhimu