1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rice aionya Korea ya Kaskazini kutofanya jaribio la pili la kinuklia

P.Martin18 Oktoba 2006

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani,Condoleezza Rice amewasili Japan kwa ziara itakayompeleka pia Korea ya Kusini,China na Urussi.

https://p.dw.com/p/CBIA
Condoleezza Rice na waziri mwenzake wa Japan Taro Aso
Condoleezza Rice na waziri mwenzake wa Japan Taro AsoPicha: AP

Wakati wa ziara yake,Rice atajadiliana na viongozi wa nchi hizo njia ya kutekeleza vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea ya Kaskazini.

Ziara ya waziri Rice inafanywa wakati ambapo kuna wasi wasi mpya kuwa Korea ya Kaskazini huenda ikawa inajitayarisha kufanya jaribio la pili la kinuklia.Rice amekwenda na mpango wenye azma ya kuhakikisha kuwa mizigo ya Korea ya Kaskazini itakaguliwa na pia kuionya serikali ya Pyongyang kutofanya jaribio la pili la kinuklia.Lengo la kukagau mizigo inayoingia na kutoka Korea ya Kaskazini kwa njia ya bahari,ardhi kavu au anga, ni kuhakikisha kuwa nchi hiyo haitouza silaha zake za kinuklia kwa magaidi au mataifa mhimili wa maovu.Maafisa wa Kimarekani wamesema,ukaguzi huo utaambatana na azmio 1718 lililopitishwa siku ya Jumamosi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya Pyongyang kufanya jaribio lake la kwanza la kinuklia.Rice alipozungumza na maripota kabla ya kuanza ziara yake alisema kuwa kuna wajibu wa kuiwekea Korea ya Kaskazini vikwazo na pia kuna wajibu wa kukagua baadhi ya mizigo.Akaongezea kuwa anaamini madola yote yanadhamiria kutimiza wajibu huo.Akaeleza kuwa atazihakikishia Japan na Korea ya Kusini kuwa nchi hizo zitalindwa na Marekani.Akiendelea alisema,njia ya kukabiliana na kitisho cha usalama ni kuwa na ushirikiano imara kama ule wa Marekani pamoja na Korea ya Kusini na Japan.Nchi hizo zinaweza kutegemea ushirikiano huo na kuwa na hakika kwamba zitalindwa dhidi ya kitisho cha hivi sasa.

Siku ya Alkhamisi atakapokwenda Seoul,waziri Rice ataiomba Korea ya Kusini ishiriki katika operesheni isiyo rasmi na kuongozwa na Marekani-PSI.Mpango huo unaendelea tangu mwaka 2003 na unaruhusu ukaguzi wa mizigo inayosafirishwa kwa meli au ndege,inaposhukiwa kuwa silaha za haramu. Afisa wa ngazi ya juu anaefuatana na Rice amesema majadiliano pamoja na serikali za nchi zote nne zinazotembelewa yatashughulika hasa na hatua za kukagua mizigo ya Korea ya Kaskazini.

Na hilo ni suala lenye utata na kupingwa na China iliyo rafiki mkuu na mshirika wa biashara wa Korea ya Kaskazini.Hata hivyo waziri Rice amesema ana imani kuwa serikali ya Beijing itatekeleza kinachohitajiwa.

China,Japan,Urussi na Korea ya Kusini ni washirika wa Marekani katika majadiliano na Korea ya Kaskazini ambayo yamekwama.Majadiliano hayo yana azma ya kuishawishi Korea ya Kaskazini kuachilia mbali mradi wake wa kinuklia na badala yake itapewa msaada wa kiuchumi na kisiasa.Waziri Rice amesema Korea ya Kaskazini itazidi kutengwa ikiwa itafanya jaribio la pili la kinuklia. Amesema hakuna anaetaka kuona mgogoro wa sasa kuwa mkubwa zaidi na mlango upo wazi kwa Korea ya Kusini kurejea katika meza ya majadiliano bila ya masharti.