1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shabulio la Kabul laaniwa dunaini

Kalyango Siraj7 Julai 2008

Ujerumani yasema ni tisho kwa demokrasia

https://p.dw.com/p/EXm4
Polisi wa Afghanistan wakishika doria nje ya ubalozi wa India mjini Kabul ulioshambuliwa na bomu. Shambulio limelaaniwa kote duniani.Picha: AP

Shambulio la Ubalozi wa India mjini Kabul nchini Afghanistan ambalo limewauwa watu zaidi 40 na kuwajeruhi wengine 141, wengi wakiwa ni raia wa kawaida, limelaaniwa ndani na nje ya nchi hiyo.

Shambulio hilo la kujitoa mhanga ambalo limetokea jumatatu asubuhi linaaminiwa kufanywa na wapiganaji wa Kitaliban.

Ujerumani ni miongoni mwa mataifa ambayo yamelaani vikali shambulio hilo katika ubalozi wa India mjini Kabul.

Katika taarifa iliotolewa na waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier,serikali ya Berlin, imelaani shambulio hilo na kutaka kukamatwa mara moja kwa waliohusika na shambulio hilo.Aidha imesema kuwa ,lengo la magaidi hao ni kuzuia kuleta hali ya kidemokrasia nchini Afghanistan.

Ujerumani inachukua nafasi ya tatu kati ya mataifa ya kigeni yaliyochangia majeshi nchini Afghanistan.

Mwezi uliopita baraza la mawaziri la Ujerumani lilikubali kuongeza idadi ya askari wake nchini huko ambao wako katika eneo tulivu la kaskazini mwa Afghanistan.

Wanajeshi waliongozwa kutoka 1,000 hadi 4,500.

Afisa mmoja wa serikali ya Afghanistan amesema kuwa shambulio hilo lilifanywa kwa ushirikiano na mojawapo wa vikosi vya ujasusi vya kikanda.Inaelekea alikuwa vinyoshea kidole vikosi vya Pakistan ambavyo vina watu ambao wanawaunga mkono wapiganaji wa Kitaliban.

Rais Hamid Karzai amawalaumu aliowaita maadui wa uhusiano mzuri kati ya nchi yake na India.maafisa wa Afghanistan hapo kabala wameilaumu Islamabad kwa kuwapa hifadhi wapiganaji wa Kitaliban.

Lakini Pakistan kwa upande wake imelaani shambulio la jumatatu ambalo limewauwa watu 41 kwa habari za hivi punde.Taarifa iliotolewa na waziri wa mashauri ya kigeni wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi, imesema kuwa Pakistan inalaani ugaidi wa aina yoyote ile ambao unatishia maisha ya mwanadamu.

Serikali ya Indonesia nayo imelaani shambulio hilo ambalo pia limewauwa walinzi watano wa ubalozi wake na pia kuwajeruhi wanadiplomasia wake wawili.

Rais Susilo Bambang Yudhoyono ametuma risala za rambirambi kwa jamaa wa walinzi hao ambao walikuwa raia wa Afghanistan.

Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Indonesia,Teuku Faizasyah,amehakikisha tukio hilo la kusema kuwa ubalozi wake umeharibiwa na shambulio hilo.Aidha amesema kuwa ingawa ubalozi wake haukuwa shabaha ya shambulio hilo lakini mlipuko ulitokea karibu na ubalozi huo.

Marekani pamoja na India nazo zimelaani shambulio hilo.Shambulio hilo limetokea jumatatu asubuhi wakati gari moja lililokuwa na baruti kugonga mlango ya ubalozi huo.Mlipuko huo uliwauwa watu zaidi ya 40 na kuwajeruhi wengine 141.

Mbali na maafisa wawili wa ubalizi wa India mkiwemo muambata wa kijeshi kuuawa lakini wengi wa wahanga walikuwa raia wa kawaida ambao walikuwa wanasubiri kupewa kibali cha kusafirria kwenda India.

Kundi la Taliban ndio linalaumiwa kuhusika ingawa kwa upande wake limekanusha.