1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TAMASHA LA 26 LA BAGAMOYO NA MCHEZO WA FISI.

Christopher Buke25 Oktoba 2007

Mwarabu anacheka Shilole anaishia kumtizama.

https://p.dw.com/p/C7rc

“ Eti fisi leo anapigiwa ngoma anacheza?”, aliniuliza kijana mmoja aliyesogelea kwa haraka nilipokuwa. Muda wa kumpa maelezo marefu ulikuwa hautoshi kwa hiyo nikamjibu kwa ufupi “ na mimi nasikia hivyo”.

Inaelekea kijana yule alikuwa angali na hamu ya kuniuliza maswali mengi zaidi lakini hakuendelea. Pengine kasoma hisia zangu kuwa wakati huo na mimi nahangaika na mikrofoni yangu huku nikitathmini eneo litakalonifaa kunasa sauti kwa ufanisi.

Tamasha la Bagamoyo la mwaka huu ambalo ni la 26 lilivuma sana na kuwahamasisha wengi. Bila shaka ni kutokana na vimbweka, raha na uhondo ambavyo watu hupata wakati wa matamasha kama haya kwa miaka iliyopita, maana tamasha kama hili hufanyika kila mwaka.

Lakini kwa upande mwingine watu walihamasika sana kuja kuona fisi akicheza ngoma. Waliambiwa na mapema na tena fisi huyu alitangazwa kuwa angechezeshwa wakati wa tamasha la mwaka jana ikashindikana kwa hiyo kuambiwa kuwa tamasha la mwaka huu fisi yupo nani akose?

Haya, wakati tunaendelea kusubiri onyesho kuanza rasmi niliwasogelea wasanii wa kikundi hiki cha kutoka mkoani mwanza ili kujua wasifu wa fisi hawa. Fisi wacheza ngoma.

Ndipo wasanii hao wakaanza kunifahamisha mengi. Kwa hapa nyumbani wanyama hawa kwa kiasi kikubwa wanahusishwa na imani za ushirikina. Ukimtaja fisi huna tofauti na mtu aliyemtaja bundi.

Msimamizi akathibitisha kuwa sio mmoja bali wameleta fisi wawili. Na akaniambia kabisa kuwa fisi hao wana majina. Mmoja anaitwa shilole ambaye ni mkubwa na mwenye madoa mengi yanayoelekea kuwa kama ya chui, na mdogo anaitwa mwarabu. Na mwarabu sio kwamba madoa hana. Anayo lakini haidhuru si mengi kama ya shilole.

Shilole ana umri wa miaka 8 wakati mwarabu ana mika 6. wasanii hawa wanadai shilole na mwarabu hula nyama lakini hata ugali kwa dagaa wakisongewa wanakula, alimradi kila mmoja apate jumla ya kilo nne kutwa.

Kilichonigutua zaidi kilitokana na swali nililowauliza kuwa nani jike au dume. “Hawa Bwana kila mmoja ana maumbile ya kike na kiume”ananifahamisha msanii. Ndipo nikahoji tena “sasa mnawatambuaje fisi dume na jike?”.

Nikaambiwa wanapofikia hitaji la kupata watoto basi wanyama hawa hupigana na yule anayeshindwa au kuishiwa nguvu basi ndiye anapandwa na panapouwezekano anabeba mamba na kisha kuzaa.

Basi maelezo hayo yakaja kukatizwa na mtangazaji wengine wakimwita MC, ambaye sasa anaashiria kuanza tamasha la 26 la Sanaa Baagamoyo na Utamaduni wa Mtanzania.

Baada ya kwaya maalumu iliyoandaliwa kutumbuiza wimbo maalumu na baada ya waheshimiwa viongozi kutoa nasaha zao mbalimbali hatimaye mirindimo yenye vionjo vya kila namna ikaanza.

Kikundi cha JKT Ruvu kikafungua uwanja kwa wengine hali hiyo wakiita kupasha moto jukwaa. Lo! Kina wachezaji machachari, hawashikiki wale.

Basi wakamaliza onyesho wakashangiliwa pale ikaisha. Watu wametulia tuli! Wanamsubiri fisi apigiwe ngoma acheze tena washaambiwa fisi mwenyewe si mmoja ni wawili. Lakini mara hii likaingia onyesho la sarakasi. Watu kama ilivyoada wakashangilia wakesha.

Mara hii MC anawatangazia watazamaji kuwa “sasa kinafuata kikundi cha kutoka Geita Mkoani mwanza na fisi uwanjani”, basi wenye vigeregere wanapiga nderemo usiseme na miguno vile vile inasikika.

Mara askari wa mgambo anawaonya waliokaa safu ya mbele ambao wengi wao watoto wadogo na sisi mapaparazzi “ mbele msikae waoga mbele msikae waoga”. Wengine wanambeza lakini wengine wanaanza kusogea nyuma kweli.

Kwa mwenye kuzifahamu ngoma za kisukuma au aliwahi kuzisikia midundo yake ni tofauti na ngoza za makabila mengi. Kidogo sauti ya milio ya ngoma zile inaogofya. Kweli zikaanza kupigwa huku wasanii wa kikundi kile wakicheza. Mtu anacheza utadhani kwa taratibu lakini kwa kutumia nguvu.

Mara wanaingia wazee wawili wa kisukuma uwanjani mmoja akiwa na dawa nyeusi iliyozongwa-zongwa kwenye karatasi la nailoni. Anaanza kunyunyizia dawa ile kama anatambikia.

Kadiri anavyominimina ndivyo na midundo ya ngoma inavyozidi kuhanikiza.

Mara sanduku linasogezwa ki-aina aina karibu na jukwaa. Watu wanachachawa na mzee anaendelea kumimina dawa zake.

Mwanamume na mwanamke waliokaa karibu yangu wanaanza kunong’onezana. “ Anamimina nini?” anauliza mwanamke, ambaye anajibiwa na yule mwenziwe “ Ule ni uchawi anatambikia! we unadhani mchezo umlete fisi acheze ngoma? we vipi?” kinapita kicheko kwa taratibu.

Haya! hayawi hayawi mwishowe yanakuwa.

Mara komeo la sanduku lingine linafunguliwa lakini kumbe mle hakuwemo fisi bali joka kubwa. Alimuradi mwenzangu. Basi linabebwa joka lile nakwambia huku ndo kwanza wale wasanii wakipiga magoma yao kama vile sasa hawana jinsi.

Kumbe kuna masanduku mawili! Mara hata lile la pili linafunguliwa na yule mzee mmimina dawa anasimama juu ya sanduku lile. Makomeo yake yanafunguliwa. Kelele za shangwe zilizochanganyikana na woga zinasikika. fisi yuleee anatoka.

He! kumbe kweli? Nkamuona fisi anachoropoka kutoka kwenye ule msanduku. Kwa maelezo niliyopewa kabla nikajua kuwa shilole yuleeee!

Kazi ikaanza ya kumtoa mwarabu. Mwarabu bwana hajataka kutoka. Basi kukuru kakara mwishowe akatoka na ndo goma likakolea likapigwa kweli na wanenguaji wakazidisha umahiri.

Mara kijana mmoja miongoni mwa wasanii kamg’ang’ania mwarabu. Kamkaba mgongoni huku anavuta mnyororo alofungiwa utadhani wana visa. Watu wakamsihi kijana yule amwachie mwarabu japo acheze ngoma kidogo, wapi! Yeye kamg’ang’ania. Mwishowe mwarabu kafungua makanwa yake meno hayooo! nje. MC naye kwa mzaha wake kadai mwarabu anacheka lakini watazamaji wakadai ameogopa.

Wakati ubishi ukiwa umetanda na wasikilizaji wakizidi kuhanikiza mwarabu aachiwe acheze lo Mwarabu Bahati mbaya akajisaidia hadharani, pale jukwaani. Wale wenye kujua mambo ya bagamoyo wakaona ndio basi tena.

Kumbe hilo na yule mzee anayemimina zile dawa kama alikuwepo. Mara moja anaamrisha mwarabu aachiwe na bila ajizi yule fisi mdogo anachoropoka na kurudi kwenye msanduku.

Shilole ambaye kwa muda akiangalia yote anayotendewa mwarabu naye hakuona la muhimu zaidi ya kuchupa na kujitoma kwenye banda lao. Na ngoma ikaisha.

Haya ndiyo mambo ya asili mpenzi wa Deutsche Welle na tena kama ambavyo wengine wajigamba kuwa hapa ni Bagamoyo. Hili ni tamasha la 26 la Sanaa Bagamoyo na Utamaduni wa Mtanzania.

Kwa wale wanaojua mambo walinambia ngoma ilichezwa tena sana lakini wengine kama sie wakuja tungali tukihoji mbona fisi hakucheza bali mwarabu kaishia kucheka?

Mimi naendelea na vimbwanga vya Tamasha la Bagamoyo na utaendelea kuvipata kadiri vinavyojiri. Wasalaam.

Mwisho.