1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania, Kongo kutupa karata ya kwanza AFCON

17 Januari 2024

Timu mbili zinazoiwakilisha kanda ya Afrika Mashariki na Kati kwenye michuano ya kandanda ya mataifa barani Afrika, AFCON, zinateremka dimbani baadaye leo kwa mechi za kwanza za hatua ya makundi zote zikiwa kundi F.

https://p.dw.com/p/4bLTX
AFCON 2024
Kombe linalopambaniwa katika michuano ya AFCON Ivory CoastPicha: MOHAMED ABD EL GHANY/REUTERS

Kikosi cha Taifa Stars ya Tanzania, kitakuwa na miadi na moja ya miamba ya soka barani Afrika, timu ya taifa ya Morocco.

Taifa Stars inayoshiriki michuano ya AFCON kwa mara ya tatu itakuwa na kibarua kigumu cha kuwashinda ´Simba wa Milima ya Atlas´, walioandika historia mwaka 2022 kwa kuwa timu ya kwanza barani Afrika kutinga nusu fainali ya kombe la dunia.

Morocco ina wachezaji mahiri kama Achraf Hakimi lakini inatajwa vilevile kwamba kikosi cha Stars nacho kinao nyota walio na ari ya kuonesha kandanda safi kwenye uga wa bara zima.

Timu nyingine ya kanda hiyo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itapimana ubavu na Zambia katika mchezo mwingine wa kundi F.

Zambia ilibeba kombe la AFCON mwaka 2012. Kongo inayoshiriki michuano ya AFCON kwa mara ya 20 nayo ina historia nzuri kwani ilikwishalitwaa taji hilo mara mbili mnamo mwaka 1968 na 1974. 

Wakaazi wa Afrika Mashariki na Kati bila shaka wataketi mbele ya runinga zao kutizama timu gani kati ya Kongo au Tanzania itakayowatoa kimasomaso.

Namibia yaishangaza Tunisia kwa kichapo cha bao 1-0 mchezo wa kundi E

Katika michezo ya hapo jana usiku Namibia na timu ya soka ya Tunisia ziliteremka dimbani na Namibia kuibuka na ushindi wa kustaajabisha wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa kombe la AFCON.

Mchezo kati ya Namibia na Tunisia
Mchezo kati ya Namibia na Tunisia uliomalizika kwa bao 1-0.Picha: AMADA MASARU/Shengolpixs/IMAGO Images

Ulikuwa ushindi wa kwanza wa kihistoria wa Namibia kwenye michuano hiyo ya kandanda barani Afrika.

Timu hiyo ilikwishaonesha makali tangu kwenye mechi za kufuzu kushiriki AFCON pale ilipoifunga mara moja na kisha kutoa sare kwenye mchezo mwingine na Cameroon, ambayo ni moja ya timu vigogo za soka barani Afrika.

Katika mchezo wake wa jana ilikuwa ni mshambuliaji Deon Hotto ndiye alipachika wavuni bao la ushindi la Namibia mnamo dakika ya 88 na kuwaacha Tunisia mdomo wazi wasiamini kilichotokea.

Tunisia iliyopoteza mchezo mbele ya Namibia jana iko nafasi ya tatu katika viwango vya ubora wa soka barani Afrika na kulambishwa kwao mchanga kumedhihirisha kuwa michuano ya safari hii alau katika hatua ya makundi bado haina mbabe.

Hakuna mbabe hatua ya makundi lakini Mali yailambisha shubiri Bafana Bafana

AFCON| Mali vs Afrika Kusini
Wachezaji wa Mali wakishangilia moja ya mabao waliyofunga kwenye mchezo na Afrika Kusini.Picha: Luc Gnago/REUTERS

Ushindi wa Namibia mbele ye Tunisia ni matokeo mengine ya kushangaza kwa timu mahiri za soka barani Afrika kupoteza mchezo katika hatua ya makundi.

Kwanza ilikuwa ni Nigeria mnamo Jumapili iliyopita, ambayo ilishindwa kufurukuta mbele ya Guinea ya Ikweta. Misri ya Mohamed Salah iliponea chupuchupu kupata idhara na kulazimisha sare ya 2-2 ilipokutana na Msumbiji.

Cape Verde iliishinda Ghana, timu ambayo imekuwa na mafanikio makubwa kwenye mchezo wa soka barani Afrika, ikiwa na historia ya kubeba makombe manne ya michuano ya AFCON.

Siku ya Jumatatu, miamba Cameroon nayo ililazimishwa sare ya 1-1 ilipokutana na Guinea kabla ya Algeria nayo kuambulia sare kama hiyo kwenye mchezo wake dhidi ya Angola.

Namibia sasa inashika nafasi ya pili kwenye kundi E nyuma ya Mali ambayo iliibamiza Afrika Kusini bao 2-0 kwenye mchezo mwingine wa kundi hilo uliochezwa usiku wa kuamkia leo.

Mali ilifunga mabao yote mawili ndani ya dakika sita za kwanza za kipindi cha pili. Magoli ya Hamari Traore na  Lassine Sinayoko yalitosha kuipa kilio kisicho na mwenyewe timu ya Bafana Bafana iliyo na rikodi dhaifu kwenye michuano ya AFCON katika miaka ya karibuni.