1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

THE HAGUE: Mwanajeshi wa Uholanzi auwawa

27 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBVW

Kamanda wa jeshi la Uholanzi amethibitisha leo kwamba mwanajeshi mmoja wa nchi hiyo aliuwawa kwenye mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara karibu na mji wa Deh Rawod kusini mwa Afghanistan.

Jenerali Dick Berlijn amewaambia waandishi wa habari mjini The Hague kwamba mwanajeshi huyo mwenye umri wa miaka 30 aliuwawa wakati alipokuwa akihudumu nchini Afghanistan kama sehemu ya kikosi cha Uholanzi katika jeshi la jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi, NATO.

Mwanajeshi mwengine wa Uholanzi alijeruhiwa katika mlipuko huo. Sambamba na taarifa hiyo, jeshi la jumuiya ya NATO nchini Afghanistan limelilaumu kundi la Taliban kwa kuripoti habari za uongo kuhusu idadi ya raia wanaojeruhiwa.

Viongozi nchini Afghanistan wanadai raia 18 waliuwawa jana na wanajeshi wa jeshi la muungano mkoani Helmand, ambao ni ngome ya mwanamgambo wa kundi la Taliban.

Msemaji wa jeshi la ISAF nchini humo, kapteni Vanessa Bowman, amesema kuna ushahidi unaodhihirisha kwamba madai hayo yalibuniwa kama sehemu ya propaganda dhidi ya serikali ya Afghanistan na vikosi vya kimataifa nchini humo.