1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Tumejitolea sana kupita kiasi" - Sarkozy

28 Oktoba 2011

Baada ya mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya uliofanya maamuzi makubwa kuhusiana na mfuko wa kuinusuru Kanda ya Euro, Rais wa Nicolas Sarkozy wa Ufaransa asema wamejitolea sana na sasa lazima wafanye kazi sana.

https://p.dw.com/p/130hU
Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: picture-alliance/dpa

Ni katika mahojiano ya jana (27.10.2011) na kituo cha televisheni mjini Paris, ambapo Sarkozy alitoa kauli hiyo. Habari muhimu kwa Wafaransa ikiwa ni kwamba serikali yao inalazimika kuzidi kubana mkanda. Sarkozy alihitaji dakika 42 kumtoa paka huyo kwenye gunia.

"Ili tuwe makini, tutatakiwa kufanya yale marafiki zetu wa Ujerumani walichokipitia, kupanda kwa asilimia moja kwa mwaka mzima ujao. Maana yake ni kuwa, tunalazimika kukata matumizi ya ndani, tunalazimika kupata kati ya euro bilioni sita hadi nane." Alisema Sarkozy.

Mtu angelishuku ni kwa kiasi gani serikali inaweza kukusanya kodi inayoweza kufikia kiwango hicho. Lakini katika wakati ambapo mgogoro wa madeni unanukia kila upande, kila kitu kinachozalishwa, kuuzwa na kununuliwa kinajikuta kikiwa chanzo cha kukusanyia euro.

Rais Nicolas Sarkozy (kushoto) akizungumza na Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Jose Manuel Barosso.
Rais Nicolas Sarkozy (kushoto) akizungumza na Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Jose Manuel Barosso.Picha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, katika mahojiano haya ya jana, Rais Sarkozy amekiri kwamba ukatwaji wa kodi hauwezi kuwa wa jumla-jamala, maana ikiwa hata vinywaji baridi vitapandishiwa kodi yake, basi mwisho wa siku mtumiaji wa kawaida nchini Ufaransa atajikuta amefilisika, na hilo, kwa maneno ya mwenyewe Sarkozy, "si haki!"

Kwa jumla, mahojiano hayo na kiongozi wa nchi yalikuwa kama darasa kwa raia wa Ufaransa, likiwafahamisha utandu na ukoko wa kile kilichofikiwa kwenye mkutano wa jana Brussels na kipi wao, kama sehemu ya wakaazi wa Kanda ya Euro, wanapaswa kukitegemea.

Ndio maana Rais Sarkozy, alizungumzia kwa urefu kuhusiana na mifuko ya dhamana, uwezekano wa kuitegemea China, ambao yeye hauamini, na jukumu la Ulaya kama familia moja, ambapo haiwezekani kuitenga Ugiriki.

Wengine wanayachukulia yote haya kuwa ni sehemu ya juhudi za Sarkozy kupigania muhula mwengine wa uraisi. Ndio maana kuna sentensi nyengine kwenye mahojiano haya zilielekezwa moja kwa moja kwenye ushawishi na kujitetea.

Marine Le Pen
Marine Le PenPicha: DW

Ndio maana pia, baada ya mahojiano haya, Idara ya Mawasiliano ya Ikulu ilitoa taarifa inayoorodhesha muhtasari wa aliyoyazungumza Rais Sarkozy, waandishi waliofanyiana naye mahojiano na maswali yaliyoulizwa.

Chama cha Sarkozy, UMP, kimeyachukulia na kimeyaita mahojiano haya kama ni hotuba ya Rais kwa taifa, lakini wapinzani wao, kama vile Marine Le Pen, mwanasiasa wa mrengo wa kulia, Rais Sarkozy amejimaliza zaidi kwa mahojiano haya, na sio kujijenga.

"Ningeliweza kuichukulia kuwa ya maana, kama angelikuwa tayari yeye ni mgombea rasmi wa chama chake. Lakini kampeni zinaanza mwezi wa Februari, na hadi kufika kwenye uchaguzi, anajiniumiza mwenyewe tu." Amesema Le Pen.

Lakini naye Sarkozy hataki kuupalilia upinzani kama huo. Maana ni kweli bado hajasema ikiwa atagombea au la.

Mwandishi: Johannes Duchrow/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo