1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia kuunda serikali mpya

Halima Nyanza17 Januari 2011

Uongozi wa mpito nchini Tunisia leo unajiandaa kuunda serikali mpya ya umoja wa kitaifa, baada ya wanajeshi kupambana na kikosi kilichokuwa kikimlinda Rais aliyeondoka madarakani Zine El Abidine Ben Ali karibu na Ikulu.

https://p.dw.com/p/zyd3
Rais wa muda wa Tunisia, Fouad Mebazaa
Rais wa muda wa Tunisia, Fouad MebazaaPicha: AP

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tunisia cha Progressive Democratic (PDP), Maya Jribi, amesema serikali hiyo mpya itakayoundwa itajumuisha mawaziri kutoka chama cha rais wa zamani, wanachama wa upinzani na viongozi wengine wa kujitegemea.

Lakini kuna taarifa nyengine zinazosema kwamba mawaziri kutoka chama hicho cha Zine El Abidine Ben Ali, ambaye siku ya Ijumaa alikimbilia nchini Saudi Arabia baada ya maandamano makubwa yaliyofanyika nchini humo dhidi ya utawala wake, hawatokuwemo katika serikali hiyo ya umoja wa taifa, wala vyama vilivyokua karibu na utawala huo wa zamani.

Amesisitiza kusema kuwa uamuzi wa kutovijumuisha vyama hivyo ni kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.

Jeshi lapambana na wafuasi wa Ben Ali

Wakati vyama vya upinzani vikijiandaa kuunda serikali, duru za polisi zinasema kwamba jeshi la nchi hiyo limefanya mashambulio katika maeneo ambayo walinzi wa rais huyo wa zamani, Ben Ali wamekimbilia.

Aliyekuwa rais wa Tunisia, Zine Al Abidine Ben Ali
Aliyekuwa rais wa Tunisia, Zine Al Abidine Ben AliPicha: picture-alliance/dpa

Aidha majeshi hayo ya ulinzi pia yaliwaua watu wawili waliokuwa na silaha, ambao walikuwa wamejificha jirani na Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi hiyo katika mji mkuu wa nchi hiyo Tunis na pia kushambuliana kwa risasi na watu wengine waliokuwa na risasi ambao walikuwa karibu na makao makuu ya chama kikuu cha upinzani nchini humo cha PDP.

Waziri mkuu wa Tunisia Mohammed Ghannouchi ameonya kwamba hakutakuwa na uvumilivu kwa yeyote yule atakayetishia usalama wa nchi na kusema kuwa serikali mpya ya taifa hilo la Afrika ya kaskazini "inaweza" kutangazwa leo.

Ujerumani yasisitiza demokrasia zaidi

Katika hatua nyingine Ujerumani imesisitiza umuhimu wa kuwepo demokrasia ya kweli katika kipindi hiki cha mabadiliko nchini Tunisia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: dapd

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema nchi yake itatumia ushawishi iliyonayo kisiasa kuhakikisha Tunisia inaelekea katika Demokrasia.

Naye, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amesema nchi yake imetiwa moyo na kauli za Waziri mkuu wa Tunisia pamoja na Rais wa mpito Foued Mebazaa, ambaye pia ni Spika wa bunge la nchi hiyo, kwa ushirikiano wao waliouonesha katika kuunda serikali hiyo mpya.

Waziri mkuu wa Tunisia amekuwa akishauriana na viongozi wa vyama vikuu vya upinzani mjini Tunis juu ya muundo wa serikali hiyo ya umoja wa kitaifa ili kuziba pengo lililoachwa na Ben Ali aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 23.

Wakati huohuo mwanasiasa wa Tunisia wa mrengo wa kushoto asiyeelemea katika msimamo wa kidini, Moncef Marzouki amesema atawania nafasi ya Urais katika uchaguzi ujao.

Chama chake cha Congress for the Republic -CPR- kilipigwa marufuku chini ya utawala wa Rais Ben Ali.

Uchaguzi nchini humo unapaswa kufanyika katika kipindi cha siku 60 tangu kuapishwa rais wa mpito mwishoni mwa juma lililopita.

Mwandishi: Halima Nyanza/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman