1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasitisha ushiriki katika Mkataba wa Silaha.

Mohamed Dahman14 Julai 2007

Urusi inasitisha ushiriki wake kwenye mkataba muhimu wa kudhibiti silaha ambao unaweka vikomo katika uwekaji wa wanajeshi barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/CB2p
Rais Vladimir Putin akiwa katika mavazi ya kijeshi.
Rais Vladimir Putin akiwa katika mavazi ya kijeshi.Picha: AP

Rais Vladimir Putin amesaini agizo lenye kuisitisha Urusi kuutekeleza mkataba huo wa mwaka 1990 wa Majeshi ya Kawaida barani Ulaya ambao unadhibiti silaha kwa kutokana na kile ilichosema kwamba mazingira yasio ya kawaida yenye kuathiri usalama wa nchi hiyo.

Mkataba huo unapunguza uwekaji wa vifaru na vikosi katika nchi wanachama za Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO na Umoja wa zamani wa WARSAW wa nchi za Ulaya ya mashariki na kuanzisha hatua zenye lengo la kujenga imani uwazi, na ushirikiano kati ya nchi wanachama.

Msemaji wa NATO mshirika wa Urusi katika mkataba huo James Appathurai ameuelezea uamuzi huo kuwa wa kukatisha tamaa na wa kurudi nyuma.

Msemaji huyo wa NATO anasema mkataba huo ni muhimu sana kwa sababu unaweka vikomo mahala ambapo watu huweka vifaru na silaha za aina nyengine pamoja na kuweka uwazi ambapo kila mtu anafahamu kile kinachofanywa na mwengine na ni kwa sababu hiyo NATO inafikiri mkataba huo ni mhimili wa utulivu barani Ulaya kutokana na kila mtu kujuwa kile kinachoendelea linapokuja suala la wanajeshi wa kawaida.

Urusi ilikuwa imetishia mara kadhaa kujitowa kwenye mkataba huo venginevyo nchi zote wanachama wa NATO zinauridhia na huku kukiwa na mashaka juu ya mpango wa Marekani wa kuweka makombora ya kujihami nchini Poland na Czeck.

Marekani na NATO zimekuwa zikitaka Urusi iondowe wanajeshi wake kutoka majimbo yake ya zamani ya Moldova na Georgia.