1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vuguvugu la kuwapinga wanajeshi Misri lazidi.

21 Novemba 2011

Waandamanaji Misri waendelea na vuguvugu za kuwapinga watawala wa kijeshi, wakidai utaratibu wa kukabidhi madaraka kwa raia uharakishwe huku idadi ya waliofariki ikiongezeka

https://p.dw.com/p/13EWp
Waandamanaji nchini MisriPicha: picture-alliance/dpa

Waandamanaji hao waliojawa na hamaki na kuzunguka uwanja wa Tahrir walilalamika juu ya utawala wa jeshi nchini humo kuchelewesha hatua ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia. Katika ghasia za maandamano hayo watu 35 wameuwawa na wengine 1,500 kujeruhiwa vibaya. Wizara ya afya nchini Misri imethibitisha vifo hivyo.

Waandamanaji hao walianza kuzua vurugu karibu na wizara ya ya usalama wa ndani nchini humo ilio karibu na uwanja wa Tahrir. Walioshuhudia wamesema maafisa wa vikosi vya usalama waliwarushia vitoa machozi na mawe waandamanaji huku waandamanaji nao wakijibu mashambulizi kwa kurusha mawe. Katika makabiliano hayo waandamanaji wanne pamoja na afisa mmoja wa usalama walijeruhiwa.

Meja Said Abbas naibu mkuu wa jeshi la kati amesema ghasia zilianza wakati waandamanaji walipofika karibu na wizara ya usalama wa ndani, Abbas amesema vikosi ambavyo havijajihami viko tayari kufika katika uwanja wa Tahrir ili kuwalinda waandamanaji.

Ägypten Demonstration am Tahir Platz in Kairo Proteste von Tunis bis Bagdad
Waandamanaji katika uwanja wa TahrirPicha: dapd

Hali hii katika uwanja wa Tahrir inafanana na ule uasi wa umma wa siku 18 mfululizo uliotokea mahala hapo dhidi ya utawala wa rais wa zamani, Mohamed Hosni Mubarak, mapema mwaka huu na kufanikiwa kumng'atua madarakani.

Ghasia hizi zimetokea wakati ambapo imesalia wiki moja kabla ya Wamisri kupiga kura kulichagua bunge jipya tarehe 28 mwezi huu.

Huku hayo yakiarifiwa bei katika soko la hisa nchini humo imeporomoka kwa asilimia 4 nukta 4 hii leo. Kwengineko Jumuiya ya nchi za kiarabu imetaka kusitishwa kwa mapigano nchini humo na kudumishwa amani. Kiongozi wa Jumuiya hiyo Nabil al-Arabi amevitaka vikosi yvote vya kisiasa kuendelea na shughuli za kuwepo kwa demokrasia nchini humo.

Syrien Arabische Liga
Wanachama wa Jumuiya ya nchi za kiarabuPicha: dapd

Ujerumani kwa upande wake umetahadharisha pande zote mbili za upinzani na utawala wa kijeshi kuwa iwapo hawatasitisha ghasia nchini humo watakuwa wanayumbisha hatua ya kupatikana kwa demokrasia nchini humo. Kupitia msemaji wa waziri wa mambo ya kigeni nchini Ujerumani Guido Westerwelle, matokeo ya matumizi ya nguvu kwa waandamanaji ni kusababisha vifo na majeruhi zaidi.

Umoja wa ulaya nao umeutaka utawala nchini Misri kuheshimu haki za kibinaadam na kutoa wito wa kusimamisha mapigano na kuwa na utulivu nchini humo, huku ukilaani matumizi ya nguvu yanayotumiwa na vikosi vya usalama kwa waandamanaji. Kulingana na msemaji wa mkuu wa mambo ya kigeni wa umoja huo Catherine Ashton, wanaangalia mambo yanavyokwenda kwa karibu sana na kutaka amani idumishwe mara moja ili kutoa nafasi kwa uchaguzi wa ubunge unaotarajiwa wiki ijayo.

Mwandishi Amina Abubakar/DPAE/AFPE

Mhariri Josephat Charo