1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Finali ya Kombe la CECAFA (KAGAME CUP) leo mjini Kigali

28 Mei 2010

Nani atatoroka na Kombe na kitita cha dala milioni 1?

https://p.dw.com/p/NcK8
Joachim Loew -amteua Lahm-nahodha wake.Picha: AP

Mabingwa wa dunia mara 3,Ujerumani ,wana miadi Jumamosi jioni na Hungary,mjini Budapest,masaa 24 baada ya kocha Joachim Löw, kumteua Philipp Lahm, beki mshahara wa Bayern Munich,nahodha wake kwa Kombe lijalo la dunia.

Kevin-Prince Boateg ,aliemuumiza Michael Ballack wakati wa finali ya Kombe la FA , ndie atakaejaza nafasi ya Michael Essien,katika Kombe la dunia akipepea bendera ya Black Stars Ghana.

Wakati waspain wanatumai gombe-dume lao Fernando Torres,litapona na mapema kucheza Kombe la dunia ,mashabiki wa Uingereza wanavuta pumzi kwamba stadi wa Steven Gerrard, atakuwa fit kwa Afrika Kusini.

Kwa mashabiki wa kanda ya CECAFA,Jumamosi hii masikio yanategwa Kigali kwa finali ya Kombe la Kagame kati ya Timu ya Jeshi la Taifa ya Rwanda na St.Georges ya Ethiopia.Kombe litaelekea wapi ?

Finali ya Kombe la klabu bingwa kanda ya Afrika Mashariki na kati mjini Kigali: Kinyan'ganyiro hiki kilichochafuliwa kwa utovu wa nidhamu wa klabu bingwa ya Afrika TP Mazembe kimefikia kilele chake jioni hii.Mshindi ataondoka sio tu na Kombe la kagame bali pia kitita cha dala milioni 1.

KOMBE LA ULAYA 2016:

Kura ilipigwa jana mjini Zurich,Uswisi kuamua wapi Kombe la Ulaya la Mataifa, 2016 litaaniwa kati ya nchi 3 zilizonyan'ganyia tiketi hiyo: Itali,Ufaransa na Uturuki:

Kura iliangukia Ufaransa, mabingwa wa dunia, 1998, kuandaa Kombe la ulaya 2016.Alietangaza ushindi wa Ufaransa, si mwengine,bali nahodha wa zamani wa Ufarans, ilipolitwaa Kombe la ulaya, 1984 nyumbani,Michel Platini,Rais wa sasa wa UEFA-shirikisho la dimba la Ulaya.

Ufaransa ikitazamiwa kushinda ingawa nchi hizo 3-pamoja na Itali na Uturuki zilikuwa bega kwa bega. Itali ilipigwa kumbo tayari duru ya kwanza ya upigaji kura kabla ya Ufaransa kuitimua Uturuki,isiowahi kuliandaa kombe hilo kwa kura 7 zaidi.

Ufaransa inapanga kujenga viwanja 4 vipya ,kwani idadi ya timu pia itaongezeka kutoka 16 kama itakavyokuwa katika kombe lijalo huko Poland na Ukraine na kuongezeka hadi 24.Ufaransa imepanga matumizi ya hadi Euro bilioni 1.7 na itachagua miji 9 kati ya 12.

Baada ya matatizo yalioikumba Ukraine na Poland , wenyeji wa Kombe la 2012 la Ulaya, Ufaransa, imeonekana haitakuwa na matatizo. Ufaransa, ilikwishaandaa Kombe la dunia, 1998 ilipotamba na stadi wake Zinedine Zidane na kutwaa ubingwa.Iliandaa pia Kombe la dunia 1938.

Ama kuhusu Kombe la Ulaya, mara ya kwanza Ufaransa kuliandaa ilikuwa 1960 pale lilipojulikana kwa jina la Kombe la Ulaya la Mataifa-European Nations Cup.Itali, mabingwa wa ulaya 1980 na tena 2000 walivunjika moyo kutopata fursa hii ya kuliandaa.Ilikuwa mara ya 3 kwa uturuki kupigania kuwa wenyeji wa Kombe la ulaya na mara hii tena wametoka mikono mitupu.

Wakati mabingwa mara 3 wa Dunia-Ujerumani, wanateremka uwanjani hivi jioni ya leo kupimana nguvu na Hungary mjini Budapest,wakiongozwa na Miroslav Klose kama nahodha wa leo, kocha Joachim Löw,alimaliza udhia na kumchagua jana Philipp Lahm,beki wa mabingwa Bayern kuwa nahodha wake mpya atakaeliongoza jahazi lake lisdiende mrama katika mawimbi ya Kombe la dunia nchini Afrika Kusini kati ya Juni 11 hadi finali Julai 11, mwaka huu: Ujerumani iko kundi D pamoja na Australia ,Ghana na Serbia.

Philipp Lahm kwahivyo,ndie atakaeliongoza jahazi la Ujerumani katika mawimbi ya Kombe lijalo la dunia nchini Afrika Kusini.Je, jahazi hilo bila ya nahodha wake wa zamani Michael Ballack, litavuka salama usalamini na kurudi nyumbani na Kombe la dunia hapo Julai 11 ,mwaka huu ?Hilo ndilo swali linaloulizwa na masjhabiki wengi nchini Ujerumani.

Mkosi uliikumba Ujerumani wiki chache zilizopita pale kipa wa Ujerumani na wa Bayer Leverkusen, Rene Adler, alipoumia mbavu na kubidi kuchupa nje ya jahazi hilo.Baadae, ikawa zamu ya nahodha mwenyewe Michael Ballack,kuumia kwa Ballack kuliwastua wengi,kwani jahazi bila ya nahodha, huenda mrama na mwishoe, kuzama.

Wajerumani lakini, wanadai Bastian Schweinsteiger,atajaza pengo la Ballack kama mchezaji wa kiungo na makamo nahodha nyuma ya Philipp Lahm.Isitoshe, kikosi cha Ujerumani, kina wachezaji 7 wa klabu bingwa Bayern Munich, iliolikosa chupu chupu majuzi mjini Madrid Kombe la klabu bingwa barani ulaya ilipolazwa na Inter Milan 2:0.

Pale Ujerumani 1974, ilipotamba na wachezaji 7 kutoka Bayern Munich, ,ilitoroka na Kombe la dunia nyumbani kwa kuilaza Holland mabao 2:1.Kwahivyo, hiyo ni ishara njema huko Afrika Kusini.

Ghana , ambayo iko kundi moja na Ujerumani,itabidi pia kucheza bila ya stadi wake wa kiungo,Michael Essien.Maajabu lakini, nafasi ya Essien, anachukua mchezaji yule yule aliemuumiza nahodha wa Ujerumani,Michael Ballack.Kevin-Prince Boateng, ambaye nduguye Jerome' Boateng, ataichezea Ujeruman, katika kombe la dunia na wote ni wa asili ya Ghana,ndie aliemuumiza mguu Ballack.Ilikuwa wakati wa finali ya Kombe la FA kati ya Chelsea na Portsmouth mwezi huu.

Kevin-Prince Boateng, aliwahi kuichezea timu ya vijana ya Taifa ya Ujerumani kabla kughairi na kuichezea timu ya Taifa ya Ghana,asili ya baba yake.Sijui kwahivyo, jazba zitakuwaje siku Ujerumani, itakapocheza na Ghana na Kevin-Prince Boateng, akivaa jazi ya Ghana na Jerome Boateng ,jazi ya Ujerumani?

Kwa kila hali, mpambano kati ya Ujerumani na Ghana, hapo Juni 23, utakuwa "asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu, hana budi kutia gongo.Mkutano-Nelspruit,Afrika kusini.

Mwandsihi: Ramadhan Ali/ DPAE

Imepitiwa na :Hamidou Oummilkheir