1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la dunia la rugby

Ramadhan Ali8 Oktoba 2007

Je,Springboks watatamba tena kama 1995 walipotwaa kombe hili ? Afrika kusini ilitimua j Fiji na imekata tiketi ya nusu-finali na Puma wa Argentina.

https://p.dw.com/p/C7nW

Kombe la dunia la rugby nchini Ufaransa,linafikia sasa kilele chake.Wenyeji Ufaransa, wana miadi katika nusu-finali ya kwanza na mabingwa wa dunia –Uingereza.

Kwa mashabiki wa Afrika, Springboks-timu ya taifa ya Afrika Kusini,inapigiwa upatu itaibuka mabingwa baada ya 1995 ilipotoroka na kombe hilo nyumbani.Afrika kusini ina miadi na Argentina katika nusu-finali ya pili.

Afrika Kusini –springboks wanatarajiwa ssa kutawazwa tena mabingwa tangu pale mbele ya mzeee Mandela walipotwaa taji hilo 1995 walipoliandaa nyumbani kufuatia kumalizika kwa enzi ya ubaguzi na mtengano-aparthied.

Springboks watabidi kwanza kutoana jasho na Puma wa Argentina kabla kukata tiketi yao ya finali wakitumai ama kukutana na wenyeji Ufaransa au mabingwa watetezi-Uingereza.

Kufuatia kupigwa kumbo nje na mapema kwa mabingwa mara kadhaa New Zealand na Australia,Afrika Kusini inaangaliwa ndio sasa ya kuchukua kombe.

Afrika kusini iliitoa Fiji katika robo-finali kwa mabao 37-20 wakati Argentina iliwapiga kumbo waskochi mabao 19-13.Jumamosi ijayo basi Afrika kusini itabidi ijiwinde sawa sawa kuzima vishindo vya Argentina ambayo kwa mara ya kwanza katika historia yake katika kombe la dunia la rugby,imewasili hatua hii ya nusu-finali.

Finali kati ya washindi-England-Ufaransa na Afrika kusini na Argentina itakua jumamosi ya oktoba 20.

Kwa Argentina, tayari kufika nusu-finali ya kombe hili wakati mabingwa mara kadhaa Australia na New Zealand wameshaaga mashindano ni ufanisi mkuu.

1999, Argentina ilifika robo-finali ,lakini mara hii imepiga hatua moja zaidi na nani ajuwae jumamosi inayokuja-puma waweza wakawatafuna sprinboks.Kwani, Springboks katika zahama na Fiji nusra wakione kilichomtoa kanga manyiya-walikosea mara 18 kuwazima maadui zao kutoka bahari ya pasifik.Wafiji wakitimka mbio na mpira na kuwaumiza kichwa waafrika kusini hadi pale walipopata jibu la mchezo wao.

Afrika kusini imetambua kwamba katika mpambano ujao na Argentina itabidi kuimarisha mbinu zake za kupambana na adui-tackling ama sihivyo, wamo hatarini.Si mara moja wafiji walivunja ukuta wao na kuwapita kwa kasi.

Nahodha wa Afrika kusini Smit anaungama kuwa kila kitu kimo mikononi mwao kutofanya uzembee na kurudi na Kombe la rugby Afrika kusini.

Utakumbuka ushindi wao 1995 ulifuatwa mwaka mmoja baadae,1996 na ushindi mwengine ule wa Bafana Bafana wa Kombe la Afrika la mataifa.

Ikiwa basi Springboks watawika tena mwaka huu wanapoandaa kombe lijalo la dunia 2010-la kwanza barani Afrika,nani ajuwae iwapo mfano wa 1995 na 1996, hautarudiwa tena na kombe likabaki Afrika ? Inaweza kuwa ni ndoto,lakini hakuna kisichowezekana.