1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la mataifa ya Afrika, fainali zaingia robo fainali.

Sekione Kitojo23 Januari 2010

Timu zote tano zinazoliwakilisha bara la Afrika katika fainali za kombe la dunia zimefanikiwa kuingia katika timu nane bora, licha ya kusuasua.

https://p.dw.com/p/LevT
Hassan Yebda, wa Algeria kulia akipambana na mchezaji wa Malawi Josephy Kamwendo. Algeria inapambana na Ivory Coast Jumapili katika robo fainali ya kwanza.Picha: AP

Wakati michezo ya robo fainali ya kombe la mataifa ya Afrika itakapofanyika hapo kesho Jumapili na Jumatatu nchini Angola, timu nane zilizobakia katika kinyang'anyiro hicho zitakuwa zile za kawaida pamoja na nyingine moja. Hata kama zilichechemea kuelekea katika hatua hiyo , timu zote tano wawakilishi wa bara la Afrika katika fainali za kombe la dunia zilizoko Angola, Algeria, Cameroon, Ghana, Ivory Coast na Nigeria, zimeingia katika duru hii ya timu nane za robo fainali.

Timu nyingine iliyofanikiwa kuingia katika robo fainali hiyo ni mabingwa watetezi wa kombe hilo Misri, pamoja na wenyeji Angola. Timu pekee ambaye si lazima kuwa ilitarajiwa kuingia katika duru hii ni Zambia , ambayo imejitokeza kutoka katika kundi ambalo lilijumuisha Cameroon, Tunisia na Gabon. Ushindi wa Zambia wa mabao 2-1 katika mchezo wao wa mwisho wa kundi lao dhidi ya Gabon umesababisha vijana hao wa Chipolopolo kusogea kutoka nafasi ya mwisho na kushika nafasi ya kwanza, na hivyo kuweka kile kinachosemwa kuwa ni mechi kubwa katika robo fainali.

Mchezo wa Jumatatu mjini Benguela utakuwa ni marudio ya fainali ya mwaka 2008 kati ya Mafarao wa Misri na simba wa nyika Cameroon, mpambano ambao Misr ilishinda wakati huo. Dhidi ya Cameroon , Wamisri watakuwa wanatetea rekodi yao ya kutoshindwa ya michezo 16 katika fainali hizo na ni rekodi ambayo nahodha wa Misri Ahmed Hassan anasema wachezaji wanataka kuihifadhi.

Nitajivunia sana iwapo nitakuwa nahodha wa kwanza kulinyakua kombe hili kwa mara ya tatu mfululizo. Mshambuliaji Mohamed Zidane, ambaye amerejeshwa kikosini baada ya kuomba radha kwa wachezaji wenzake pamoja na maafisa kwa kuonyesha kwake kukasirishwa baada ya kubadilishwa wakati wa mchezo, amesema kuwa michezo ya kweli sasa inaanza.

Mzaha umekwisha na kama utapoteza mchezo, unapoteza kila kitu, mshambuliaji huyo wa Borussia Dortmund nchini Ujerumani amesema.

Cameroon , ambao walisuasua na kujikwaa katika njia yao kuingia katika robo fainali hizi, wataweka ubunifu katika ndoto zao, hususan mshambuliaji wao mahiri Samuel Eto'o anayeonekana kurejea kileleni mwa kiwango chake katika wakati muafaka, kwa kufunga mara mbili katika michezo miwili ya mwisho.

Afrika Cup Tunesien Kamerun
Wachezaji wa Cameroon wanashangilia baada ya kupachika bao la pili dhidi ya Tunisia katika mchezo wao wa kundi D katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika nchini Angola.Picha: AP

Wakati huo huo kocha wa Ivory Coast Vahid Halilhodzic amesema jana kuwa timu za Afrika zinapaswa kuweka imani zaidi kwa walimu wao ili kuweza kupata mafanikio katika kiwango cha juu. Raia huyo wa Bosnia ambaye timu yake haijafungwa katika michezo 23 akiwa kama kocha wa tembo hao, tangu achukue uongozi wa timu hiyo mwaka 2008, lakini bado anahisi mbinyo mkali.

Baada ya kutoka sare bila kufungana na Burkina Faso, nilikuwa na hisia kuwa watu wananiangalia kama gaidi wakati wa mazowezi mjini Cabinda ambako timu yake inapambana na Algeria katika mchezo wa robo fainali kesho Jumapili.

Na polisi wa Angola wamepuuzia shutuma zilizotolewa na timu ya Ghana kabla ya mchezo wao wa robo fainali na wenyeji Angola. Ghana imelalamika kuwa kuna mbinu za kuwaogopesha zinazofanywa na polisi wa Angola ambazo zimepangwa wanasema kuwakatisha tamaa kabla ya mchezo wao na Angola.

Hali hiyo imepelekea mwandishi habari mmoja wa radio kutoka Ghana kupigwa na polisi wa Angola katika kile kilichoelezwa kuwa ni shambulio la kinyama. Ripota huyo Fiifi Tackie alikataliwa kuingia katika hoteli wanayoishi wachezaji wa Ghana ambao walikuwa na mkutano na waandishi habari. Mtu mmoja aliyeshuhudia ambaye pia ni mwandishi habari kutoka Ghana Frank Abdai ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa ripota huyo alikataliwa kuingia katika ukumbi wa mkutano, na alizungukwa na maafisa wa usalama na polisi na kupigwa. Alikamatwa lakini baadaye aliachiwa huru. Hayo ndio yanayotokea huko Angola pembezoni mwa viwanja vya michezo. Lakini msema kweli ni firimbi ya mwamuzi kuanzisha mapambano ya robo fainali hapo kesho.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpaT