1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiSyria

UN yasema imeafikiana na Syria kuhusu uingizaji misaada

9 Agosti 2023

Umoja wa Mataifa umesema umefikia makubaliano na Syria kupeleka misaada katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kupitia kivuko muhimu na Uturuki, hatua iliozusha wasiwasi miongoni mwa makundi ya kutoa misaada.

https://p.dw.com/p/4UxK9
USA UNO Volker Perthes New York
Picha: Manuel Elias/Xinhua/IMAGO

Makundi hayo ya kutoa misaada yalitaka serikali ya mjini Damascus isihusishwe kwenye mpango huo.

Chini ya mkataba wa 2014, misaada mingi ya kimataifa ilipitia kivuko cha Bab al-Hawa kutoka Uturuki bila idhini ya Damascus.

Hata hivyo mwezi uliopita, Baraza la Usalama lilishindwa kufikia muafaka juu ya kurefusha utaratibu huo.

Soma pia:Umoja wa Mataifa waibua wasiwasi juu ya masharti ya Syria kuruhusu misaada ya kibinadamu

Umoja wa Mataifa ulisema pendekezo lililofuata la Syria la kuweka kivuko wazi kwa miezi sita mingine lilikuwa na masharti "yasiyokubalika".

Siku ya Jumanne jioni, msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema "katibu mkuu anakaribisha maelewano yaliyofikiwa siku ya Jumatatu na Umoja wa Mataifa na serikali ya Syria, juu ya kuendelea kutumika kwa muda wa miezi sita ijayo kivuko cha mpakani cha Bab al-Hawa".

Makubaliano hayo yalifuatia mazungumzo kati ya mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths na Damascus.

Kiini cha makubaliano ni nini?

Sehemu ya makubaliano inasema kwamba Umoja wa Mataifa na washirika wake wataendelea kutoa usaidizi "katika kiwango kinachohitajika na kwa kanuni inayoruhusu mashirikiano kwa pande zote, ambazo zinalinda uhuru wa utendajiwa Umoja wa Mataifa.

Syrien | Hilfsgüter in einem Warenhaus nahe des  Bab al-Hawa Grenzübergangs
Shirika la Mpango wa Chakula WFP hupeleka nafaka SyriaPicha: Omar Haj Kadour/AFP/Getty Images

Masharti ya hapo awali ya serikali ya Syria ni pamoja na kwamba Umoja wa Mataifa ushirikiane nayo kikamilifu na sio kuwasiliana na kile ilichokiita "mashirika ya kigaidi."

Kauli hiyo ilikuwa ikilenga kundi la Hayat Tahrir al-Sham, wanajihadi ambao zamani walikuwa na uhusiano na kundi la itikadi kali la Al-Qaeda ambalo linadhibiti upande wa Syria wa Bab al -Hawa.

Soma pia:Syria: Zaidi ya muongo mmoja wa mateso na mauaji

Mashirika kadhaa ya kimataifa yameelezea wasiwasi wao kwamba, kuruhusu Damascus kudhibiti upelekwaji wa misaada katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kunaweza kusababisha kupunguza ufikiaji kwa wale walio na uhitaji zaidi.

Zaidi ya watu milioni nne wanaishi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kaskazini na kaskazini-magharibi mwa Syria, wengi wao katika kambi zilizofurika watu, na wakikosa mahitaji muhimu ya kiutu.

Kwanini mashirika ya misaada yanawasiwasi na makubaliano?

Taarifa ya Umoja wa Mataifa ilisema kwamba, idhini iliotolewa tena na Syria katika siku za hivi karibuni inatoa msingi kwa Umoja wa Mataifa na washirika wake, kufanya shughuli za upelekwaji wa misaada ya kiutu kwa kuvuka mpaka kupitia Bab al-Hawa.

Mashirika ya kutoa misaada ya kiutu yamesema kwenye tamko lao la pamoja kwamba, wana wasiwasi juu ya kutoweka kwa uhakika na usalama unaotolewa na idhini ya Baraza la Usalama kutaathiri uwezo wa mashirika hayo, na hasa yaliopo ndani ya  Syria, kufanya kazi kwa ufanisi.

Ukata wa maji Syria

Tangazo hilo la Umoja wa Mataifa limekuja saa chache baada ya taarifa kuwa Syria imeongeza kwa miezi mitatu zaidi matumizi ya vivuko vingine viwili vya Bab al-Salam na Al-Rai, ambavyo vilifunguliwa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi la Februari 6 lililopiga Syria na Uturuki na kuathiri maelfu ya wakaazi.

Soma pia:WFP kupunguza msaada wa chakula nchini Syria

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka nchini Syria baada ya serikali ya Rais Bashar al-Assad kukomesha maandamano ya amani mwaka 2011.

Mzozo huo umeua karibu watu nusu milioni na wengine mamilioni kuyakimbia makaazi yao, kabla ya vita hivyo vya wenyewe kwa wenye.

Urusi mwezi uliopita ilipiga kura ya turufu kuongezwa kwa miezi tisa kwa kutumiwa kwa utaratibu wa kivuko cha Bab al-Hawa kisha ikashindwa kukusanya kura za kutosha kupitisha nyongeza ya miezi sita.

Damascus mara kwa mara inashutumu utoaji wa misaada wa Umoja wa Mataifa kama ukiukaji wa uhuru wake.

Mshirika wake wa karibu Moscow amekuwa ikijiondoa kwenye makubaliano ya Baraza la Usalama kwa miaka sasa.