1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

100 wauawa Yemen

Angela Mdungu
2 Septemba 2019

Takriban watu 100 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mashambulio ya angani yaliofanywa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kulenga kituo cha mahabusu kinachosimamiwa na waasi wa Kihouthi nchini Yemen

https://p.dw.com/p/3OsWO
Yemen Streitkräfte Kämpfer
Picha: picture-alliance/AP Photo/Yemen Today

Shambulio hilo la angani lililofanywa na muungano wa Saudi Arabia linatajwa kuwa baya zaidi mwaka huu nchi Yemen. Kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu, shambulio hilo limewaua takriban watu 100 na kuwaacha wengine 40 wakiuguza majeraha.

Hata hivyo, muungano wa Saudia umekanusha kuwa shambulio hilo la angani lilikuwa linalenga kituo cha mahabusu na badala yake kudai kuwa shambulio hilo lililenga kambi ya jeshi.

Kiongozi wa ujumbe wa shirika la msalaba mwekundu nchini Yemen, Franz Rauchenstein anasema kuwa idadi ya vifo kutokana na shambulio hilo la angani huenda ikaongezeka. Rauchenstein, alizuru eneo la tukio jana Jumapili na kuongeza kuwa ni watu wachache tu ndio walionusurika.

Kituo hicho kilicholengwa, kipo katika eneo la Kusini Magharibi mwa wilaya ya Dhamar na kilikuwa kimehifadhi wafungwa 170.

Mjumbe maalumu wa umoja wa mataifa azitaka pande hasimu kuzungumza

Mjumbe maalum wa umoja wa mataifa nchini Yemen Martin Griffiths ametoa wito kwa pande hasimu katika mzozo wa Yemen kukaa katika meza ya mazungumzo ili kumaliza vita hivyo.

Wito huo ameutoa siku moja tu baada ya kufanya mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Sweden Margot Wallstrom katika mji mkuu wa Jordan wa Amman. Ziara ya Wallstrom mjini Amman inalenga kutafuta muafaka wa maelewano baina ya pande hasimu nchini Yemen.

Luftangriffe im Jemen
Watu wakikagua kituo cha uhifadhi wa mahabusu kilichoshambuliwa Kusini Magharibi mwa YemenPicha: picture-alliance/dpa/AP/H. Mohammed

Awali, kulikuwepo makubaliano kati ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran ili kusitisha vita na kuleta amani, japo makubaliano hayo bado hayajatekelezwa kiukamilifu.

Marekani, na muungano huo wa Saudi Arabia ambao umekuwa ukipambana na waasi wa Houthi nchini Yemen wanaoungwa mkono na Iran tangu mwezi Machi mwaka 2015, umekosolewa vikali kimataifa kutokana na mashambulizi yake kuzilenga shule, hospitali, vituo vya kujivinjari na sehemu nyengine za umma na kusababisha vifo vya maelfu ya raia wasiokuwa na hatia.

Waasi hao wa Kihouthi wanaodhibiti eneo kubwa la kaskazini mwa Yemen ikiwemo mji mkuu sanaa waliilazimu serikali inayotambuliwa kimataifa kukimbilia uhamishoni mwaka 2014.