1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

26 wauwawa katika shambulio la bomu katika hoteli Somalia

Sekione Kitojo
13 Julai 2019

Kiasi watu 26, ikiwa ni pamoja na wageni kadhaa, wameuwawa katika shambulio la bomu la kujitoa muhanga lilodaiwa na wanamgambo  wa Al-Shabaab kuwa wanahusika na shambulio hilo katika hoteli  maarufu kusini mwa Somalia.

https://p.dw.com/p/3M1z2
Somalia Angriff auf Hotel in Kismayo
Mabaki ya kifusi cha hoteli Medina mjini KismayoPicha: Getty Images/AFP

Afisa  wa  ngazi ya juu  wa  kimkoa  amesema  leo Jumamosi (13.07.2019) kuwa  mshambuliaji wa  kujitoa  muhanga  aliigonga gari iliyokuwa  na  miripuko katika  hoteli  ya  Medina katika  mji  wa bandari  wa  Kismayo jana Ijumaa  kabla  ya  watu kadhaa  wenye silaha  nzito  kulazimisha  kuingia  ndani  ya  hoteli  hiyo, wakifyatua risasi  wakati  wakiingia  ndani.

Somalia Angriff auf Hotel in Kismayo
Hoteli Maarufu ya Medina mjini Kismayo ambayo imebaki kuwa gofuPicha: Getty Images/AFP/STRINGER

Mzingiro  huo ulidumu  kwa  takriban masaa  12  na  ulimalizika  tu alfajiri  ya  Jumamosi  baada  ya  mapambano  na  majeshi  ya usalama.

Wakenya  watatu, Watanzania watatu, Wamarekani  wawili, Muingereza  mmoja  na  raia  mmoja  wa  Canada  ni  miongoni  mwa watu 26 waliouwawa  katika  shambulio  hilo, rais Ahmed Mohamed Islam wa  jimbo  lenye  mamlaka yake ya  ndani  katika  jimbo  la Jubaland amewaambia  waandishi  habaei.

"Kuna  pia  raia  wawili  wa  China  waliojeruhiwa," ameongeza.

Shirika  la  habari  la  AFP limethibitisha  pamoja  na  wana familia kuwa   kiasi ya  watu wanne waliofariki  wana  uraia  pacha.

"Majeshi ya  usalama  yana udhibiti  hivi  sasa  na  gaidi  wa  mwisho alipigwa  risasi  na  kufariki", Mohamed Abdiweli, afisa  wa  usalama alisema.

Hoteli yavamiwa

"Kuna  miili  ya  watu  waliofariki  na  ile  ya  waliojeruhiwa ikiwa imezagaa  ndani  ya  hoteli  hiyo," Abdiweli alisema.

Somalia Autobombe in Mogadischu
matukio ya mashambulizi ya mara kwa mara nchini Somalia kama hili mjini MogadishuPicha: Reuters/F. Omar

Amesema  maafisa  wanaamini  watu wanne  waliokuwa  na  silaha, ambao  mtu  mmoja  aliyeshuhudia  aliwaeleza  kuwa  walivalia  sare za  jeshi  la  polisi  la  Somalia, walihusika  katika  shambulio  hilo.

Shabaab , kundi lenye  mafungamano  na  kundi  la  al-Qaeda , limedai  kuhusika  na  mzingiro  huo  na  kuueleza  kuwa ni "shambulio  la  mashahidi".

"Kuna  mtafaruku  ndani , niliona  miili  kadhaa  ya  watu  waliofariki ikichukuliwa  kutoka  katika  eneo  la  tukio na  watu  wanakimbia kutoka  katika  majengo  ya  karibu," Hussein Muktar  aliyeshuhudia alisema  wakati  wa  shambulio  hilo.

"Mripuko  ulikuwa  mkubwa  sana," aliongeza.

Shambulio  hilo  ni  la  hivi  karibuni  kabisa  katika  mlolongo  mrefu wa  mashambulio  ya  mabomu  na  mapambano  ya  bunduki yanayodaiwa  kufanywa  na  al-Shabaab.

Watu walioshuhudia  wamesema  miongoni  mwa  waliouwawa  ni mwanaharakati  maarufu  katika  mitandao  ya  kijamii  na  mwandishi habari  wa Somalia.

Mwandishi na mwanaharakati wauwawa

"Ndugu wa  mwandishi  habari Mohamed Sahal wamethibitisha  kifo chake  na naelezwa  kuwa  mwanaharakati  katika  mitandao  ya kijamii  Hodan Naleyeh  na  mume  wake  pia  wamefariki  katika mripuko  huo, mtu  aliyeshuhudia  Ahmed Farhan  amesema.

Chama cha  waandishi  habari nchini  Somalia  SJS kimethibitisha madai  ya  kifo  cha  mwandishi  huyo. Ni  siku  ya masikitiko makubwa  kwa  waandishi  habari  wa  Somalia," katibu  mkuu  wa chama  hicho  Ahmed Mumin  amesema  katika  taarifa.

Kwa mujibu  wa  vyanzo kadhaa, wengi  wa  wale  wanaoishi katika hoteli  hiyo walikuwa  ni  wanasiasa  na  wafanyabiashara  kabla  ya uchaguzi  ujao  wa  kimkoa.

Explosion in Mogadischu, Somalia
Wapiganaji wa al-Shabaab hushambulia mara kwa mara hoteli zinazotembelewa na wageni nchini SomaliaPicha: Reuters/F. Omar

"Jengo  lote  limekuwa  gofu, kuna miili ya watu waliokufa  na waliojeruhiwa  ambao  wametolewa  kutoka  ndani. Majeshi ya usalama  yamezuwia  eneo  lote," amesema  mtu  mmoja aliyeshuhudia  Muna Abdirahman.

Wapiganaji wa  al-Shabaab  wamepigana  kwa  zaidi  ya  muongo mmoja  kuiangusha  serikali  ya  Somalia. Kundi  hilo  la wanamgambo lilitokana  na  mahakama  za  Kiislamu ambao walikuwa  wakati  fulani  wakidhibiti  eneo  la kati  na  kusini  mwa Somalia  na  wanakadiriwa  kufikia  wapiganaji  kati  ya  5,000  na 9,000.

Mwaka 2010 kundi  la  al-Shabaab lilitangaza  utiifu  wao  kwa  al-Qaeda.

Katika  mwaka  2011 , walikimbia  maeneo  yao  ambayo  waliwahi kuyashikilia  mjini  Mogadishu, na  tangu  wakati  huo  wamepoteza maeneo  yao  mengi. Lakini  wanaendelea  kudhibiti sehemu  kubwa ya  maeneo  ya  vijijini  nchini  humo  na  wanaendelea  kupambana katika  vita  vya  chini  kwa  chini  dhidi  ya  serikali.