1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

43 wafa Zimbabwe, Msumbiji kwa kimbunga

Sylvia Mwehozi
16 Machi 2019

Watu 24 wamepoteza maisha mashariki mwa Zimbabwe, baada ya kukumbwa na kimbunga Idai kilichoambatana na mvua kubwa. Kimbunga Idai tayari kimesababisha vifo zaidi ya 100 katika nchi za Msumbiji na Malawi.

https://p.dw.com/p/3FBH9
Malawi Zyklon Idai
Picha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

Kiasi ya watu wengine 40 hawajulikani walipo nchini Zimbabwe, amearifu waziri wa mawasiliano kupitia ukurasa wa twitter. Nyumba, mitaa na mashamba vimeathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua.

Wahudumu wa uokoaji wanajaribu kulifikia eneo lililoathirika zaidi la Chimanimani karibu na mpaka na Msumbiji, lakini hata hivyo zoezi hilo limetatizika kutokana na madaraja kusombwa na maji. Takribani wakazi 500,000 katika mji wa Beira wameathirika baada ya mawasiliano na huduma ya umeme kukatika.

Mashirika ya misaada yana hofu  kwamba maelfu ya watu watakosa makaazi baada ya kimbunga hicho. Nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe ndizo zilizoathirika zaidi na kimbunga Idai. Zaidi ya wakaazi milioni 1.5 katika mataifa hayo matatu, kulingana na maafisa wa serikali na Umoja wa Mataifa.

Karte Zyklon Idai Mosambik DE
Maeneo yaliyoathirika na kimbunga Idai

Watu 70 wamejeruhiwa vibaya, kwa mujibu wa gavana wa jimbo lililoathirika la Sofala Albert Mondlane. Mji mwingine wa bandari wa Beira nchini Msumbiji nao umeathirika na kimbunga Idai ambapo uwanja wa ndege ulifungwa, umeme kukatwa na makazi mengi kuharibiwa. Kimbunga hicho kilianzia Beira Alhamis jioni na kuenea hadi maeneo ya mipakani ya Zimbabwe na Malawi.

Shule na hospitali pamoja na vituo vya polisi navyo vimeharibiwa sana. Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na lile la msalaba mwekundu wanaendelea kutoa msaada katika juhudi za uokoaji pamoja na kusambaza misaada ya chakula na dawa.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema uharibifu unatia wasiwasi na kwamba mafuriko yametatiza ndege kutua kuendelea na shughuli ya uokozi. Msemaji wa serikali ya Zimbabwe Nick Mangwana amesema hii leo kwamba watu 24 wamepoteza maisha hususan katika eneo lililoathirika zaidi la Chimanimani.

Televisheni ya Zimbabwe ZBC imeripoti kuwa watu 150 hawajulikani walipo. Jeshi la Afrika Kusini limetuma ndege na wataalamu 10 wa afya kusaidia Msumbiji na Malawi.