1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ABUJA : Uchaguzi wa rais waingizwa kwenye matata

23 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC7u

Mgombea wa chama tawala Umaru Yar’Adua anaelekea kushinda uchaguzi wa rais nchini Nigeria kutokana na matokeo ya awali leo hii lakini waangalizi wa uchaguzi huo wameulani kuwa ni pigo kwa nchi hiyo kuwa kielezo cha demokrasia barani Afrika.

Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa na wale wa ndani ya nchi wamesema uchaguzi huo umeingizwa matatani mno kutokana na kujazwa kura za bandia,umwagaji damu na uhaba wa mamilioni ya karatasi za kupigia kura.

Piere Richard Prosper wa Taasisi ya Kimataifa ya Republican amesema serikali imewaangusha wananachi wa Nigeria na kwamba uchaguzi huo katika taifa lenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika milioni 140 umeshindwa kutimiza viwango vya chini vya uchaguzi vinavyokubalika.

Kundi la Mpito la Waangalizi wa Uchaguzi la Nigeria limesema uchaguzi huo hauna budi kubatilishwa na kurudiwa tena.

Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa leo hii wakati waangalizi zaidi wa kimataifa watakapotowa maamuzi yao.

Upinzani umesema huenda ikawateremsha wafuasi wake mitaani iwapo chama tawala cha PDP kitadai kushinda.