1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ABUJA : Upinzani kuandamana dhidi ya matokeo ya uchaguzi

26 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC79

Upinzani nchini Nigeria wataungana na vyama vya wafanyakazi Ijumanne ijayo kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wenye dosari uliofanyika wiki iliopita ambao umekipa chama tawala ushindi mkubwa.

Upinzani ukioongozwa na kiongozi wa zamani wa kijeshi Muhammadu Buhari umekuwa ukitafuta hatua ya kuchukuwa baada ya kutangazwa kwamba wameshindwa katika uchaguzi wa rais na wa majimbo ambao umealaaniwa na waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kuwa ulikuwa wa udanganyifu.

Tume ya uchaguzi ilimtangaza Umaru Yar’Adua wa chama tawala cha People Demokratic kuwa mshindi wa uchaguzi huo wa rais uliofanyika Jumamosi.

Rais Olusegun Obasanjo amewataka wanaolalamika kushindwa wafikishe suala hilo mahkamani kabla ya kukabidhi madaraka hapo tarehe 29 mwezi wa Mei kutakakoadhimisha kukabidhiana madaraka kwa mara ya kwanza kutoka serikali moja ya kiraia kwenda nyengine katika nchi hiyo yenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika.