1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan yahofia ghasia kutoka kwa Taliban

Tatu Karema
9 Septemba 2019

Afghanistan inajiandaa kwa uwezekano wa ghasia kutoka kwa wataliban baada ya rais Donald Trump kuyafuta kwa ghafla mazungumzo na kundi hilo ambalo limeapa kuendeleza vita dhidi ya kile linachokiita ukaliaji wa kigeni. 

https://p.dw.com/p/3PGNo
Afghanistan Selbstmordanschlag in Kabul
Picha: Reuters/O. Sobhani

Tangazo la Trump mwishoni mwa juma ambalo halikutarajiwa lilitolewa muda mfupi kabla ya msururu wa siku muhimu nchini Afghanistan ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya kifo cha kamanda aliekuwa mpinzani mkubwa wa kundi la Taliban Ahmad Shah Massoud hii leo, siku kuu ya Ashoura inayoadhimishwa na madhehebu ya kishia na Jumatano ambayo ni kumbukumbu ya mashambulizi ya Septemba 11.

Kundi hilo la Taliban lilishambulia takriban wilaya mbili katika eneo la Kaskazini Mashariki la mkoa wa Takhar usiku kucha lakini hakukuwa na ripoti juu ya majeruhi ama waathiriwa iliyotolewa. Kundi hilo limeshambulia miji mikuu ya mikoa mitatu mapema mwezi huu wakati lilipokuwa likikamilisha makubaliano na Marekani juu ya kusitisha vita ambavyo vimedumu kwa  takriban miaka 18.

Hapo jana , msemaji wa rais wa Afghanistan Sediq Seddiqqi aliwaambia wanahabari mjini Kabul kwamba haina maana kuendeleza mazungumzo hayo ambayo hayatakuwa na mwisho mwema kuhusiana na ghasia zinazotekelezwa na kundi hilo la Taliban.  Hata hivyo waziri wa ndani wa Marekani Mike Pompeo amesema kuwa wataliban walivuka mipaka kwa kutekeleza shambulizi  la bomu lililotegwa ndani ya gari katika eneo la kidiplomasia karibu na ubalozi wa Marekani mjini Kabul na kumuuwa mwanajeshi wa Marekani na hilo ndilo lililosababisha rais Donald Trump kujiondoa katika mazungumzo hayo ya mkataba wa amani wa Afghanistan huko Camp David.

Pompeo amesema sasa itabidi kundi hilo la wataliban kubadilisha mienendo yake ijapokuwa hakusema iwapo mazungumzo hayo ya amani yatarejelewa na ni lini yatarejelewa. Waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani James Mattis, amesema lin apokuja suala la kujaribu kujadili makubaliano ya amani ya Afghanistan pamoja na Wataliaban, swali muhimu ni iwapo wanaweza kuaminiwa, akitolea mfano wa mazungumzo yaliopita ya nyukilia na Warusi, wakati ambapo Wamarekani walizungumzia kile alichokiita "imani lakini hakiki."