1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika inaweza kudhibiti soko la malighafi za nishati safi?

Lilian Mtono
19 Julai 2023

Mataifa ya Afrika na yenye utajiri mkubwa wa madini yameendelea kupiga marufuku uuzwaji nje wa madini ghafi, wakipigia debe madini hayo kuchakatwa ndani ya nchi, ili kupata faida zaidi.

https://p.dw.com/p/4U8ZX
Picha inayoonyesha madini ya Lithium ambayo ni moja ya yaliyozuiwa na Zimbabwe kusafirishwa nje.
Ulimwengu unapambana kuhakikisha unajitoa katika matumizi ya mafuta na nishati inayochafua mazingira na kusababisha ongezeko la joto.Picha: Robert Michael/dpa/picture alliance

 Kuanzia Zimbabwe, yenye utajiri mkubwa wa madini ya Lithium hadi kobalti huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mahitaji ya madini muhimu kwa ajili ya teknolojia ya nishati safi yanazidi kuongezeka, wakati mataifa mengi duniani yakiwa mbioni kuachana na matumizi ya nishati inayochafua hali ya hewa na kuongeza joto duniani.

Lakini wachambuzi katika Taasisi ya Utawala wa Maliasili (NRGI), wameonya kwamba hatua hiyo pekee na pana ya kupiga marufuku mauzo ya madini muhimu haiwezi kutosheleza kusaidia ukuaji wa uchumi unaohitajika sana barani.

Soma Zaidi: UN: Dunia inapaswa kujiandaa kwa mawimbi yanayoongezeka ya joto

Na kwa jamii ya kimataifa, Umoja wa Ulaya, umeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa vikwazo hivyo vya mauzo ya nje ya madini hayo yanayoweza kutumika kwenye teknolojia ya nishati safi, vinavyowekwa na mataifa barani Afrika.

Mataifa mengi ya Afrika ambayo ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria na Namibia wameanzisha vizuizi vikali vya mauzo ya nje ama kupiga marufuku kabisa, hii ikiwa ni kulingana na utafiti uliochapishwa mwezi Mei na Jukwaa la Maendeleo la Afrika, Africa Development Forum.

Waziri wa zamani aliyeshughulikia migodi na maendeleo ya chuma nchini Nigeria Olamilekan Adegbite, aliyeongoza juhudi za kupiga marufuku usafirishaji wa madini ghafi  mwaka 2022, alisema mataifa ya Afrika yanataka kukomesha "uporaji wa malighafi barani Afrika.

Picha inayoonyesha madini ya Kolbati yanayopatikana huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na yanayohitajika kwa kiasi kikubwa.
Ulimwengu unapambana kuhakikisha unajitoa katika matumizi ya mafuta na nishati inayochafua mazingira na kusababisha ongezeko la joto.Picha: blickwinkel/imago images

Je, hii ni fursa kwa Afrika kulidhibiti soko la madini yanayohitajika kwa nishati safi?

Licha ya kuwa mzalishaji mkuu wa mafuta yasiyosafishwa, Nigeria kwa kiasi kikubwa huagiza kutoka viwanda vya kusafisha mafuta vya nje. Kulingana na Adegbite, hatua hiyo ya marufuku ya kusafirisha madini, inaweza kuchochea usindikaji wa ndani au usafishaji kabla ya kusafirisha nje ili kuzuia uporaji kwenye sekta ya madini.

Kati ya mwaka 2017 na 2022, sekta ya nishati imekuwa chanzo kikuu cha mahitaji yaliyoongezeka mara tatu madini ya Lithium, wakati mahitaji ya kolbati yakiongezeka kwa asilimia 70, na nikeli yakipanda kwa asilimia 40 hii ikiwa ni kulingana na ripoti iliyotolewa mwezi Julai na Shirika la kimataifa la Nishati (IEA).

Mataifa mengi ya Afrika yenye utajiri wa madini mara nyingi yamejikuta yakipita katika kile kinachoonekana kama "laana ya rasilimali", na utawala mbaya unaohusishwa na "rushwa, uharibifu wa mazingira, na hata ukiukwaji wa haki za binadamu, amesema Silas Olang, mshauri katika taasisi ya NRGI. Lakini hata hivyo, anakiri kwamba kwa sasa ipo fursa ya kurekebisha mwenendo uliopo barani humo wakati ulimwengu ukitupia jicho madini ya Afrika lenye asilimia 30 ya hifadhi ya madini kote ulimwenguni yanayohitajika katika teknolojia za nishati safi.

Hatua hii ya marufuku imeibua mashaka mbele ya jamii ya kimataifa. Umoja wa Ulaya kwa mfano, hivi sasa inasaka mshirika mbadala wa madini, tofauti na China na Urusi, katika harakati zake za kukabiliana na uchafuzi wa hewa ifikapo mwaka 2050. Msemaji wa tume ya Umoja huo amesema hatua za karibuni zilizochukuliwa na Namibia ya kuzuia usafirishaji nje wa baadhi ya madini muhimu huenda ikawa imekiuka makubaliano ya pamoja ya kibiasharana sheria ya Shirika la Kimataifa la Biashara, WTO. Namibia, mnamo mwezi Juni ilipiga marufuku uuzwaji wa madini ghafi ya Lithium na madini mengine.