1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya23 Februari 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya mwanaharakati Mamphela Ramphele anaekusudia kukipa changamoto chama cha ANC, nchini Afrika Kusini na juhudi za kupambana na njaa barani Afrika.

https://p.dw.com/p/17kMI
Mamphela Ramphele, mwanaharakati wa Afrika Kusini
Mamphela Ramphele, mwanaharakati wa Afrika KusiniPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Suddeutsche Zeitung" limeandika juu ya mwanaharakati wa Afrika Kusini Mamphela Ramphele anayekusudia kumpa changamoto Rais Jacob Zuma. Je, mwanaharakati huyo ni nani? Gazeti hilo linatueleza zaidi.

"Mamphela Ramphele ni mtu aliyefikiria juu ya kila kitu kwa makini - wakati, mahala na mavazi." Gazeti la "Suddeutsche"linasema Jumatatu iliyopita, mwanaharakati huyo alienda kwenye gereza la zamani ambako wanawake walifungwa, katika mji wa Johannesburg. Ni mahala hapo ambako utawala wa kibaguzi uliwatesa watu. Ni mahala hapo ambako leo ni makao ya Mahakama ya Katiba ya Afrika ya kusini.

Gazeti la"Süddeutsche Zeitung" linaeleza katika makala yake kwamba ni mahala hapo panapoitwa Constitutional Hill, ambako mwanaharakati Maphela Ramphele alipachagua kuanzisha kampeni yake ya kisiasa. Ni hapo ambapo Mamphela aliwakumbusha watu wa Afrika Kusini juu ya mapambazuko ya demokrasia. Aliwauliza "Je, mnakumbuka ndoto yetu ya kujenga jamii kubwa ya kidemokrasia nchini Afrika Kusini?" Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" limemkariri mwanaharakati huyo akisema kuwa matumaini ya kuijenga jamii kubwa ya haki yametoweka.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" limearifu katika makala yake kuwa Mamphela Ramphele anakusudia kuunda chama chake cha kisiasa na kusimama katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mnamo mwaka 2014, ili kumpa changamoto Rais Jacob Zuma. Lakini gazeti hilo limesema kwanza mwanaharakati huyo anahitaji kuungwa mkono katika ngazi ya mashinani.

Mishahara mikubwa ya wanasiasa

Gazeti la"Neues Deutschland "wiki hii limechapisha makala juu ya harakati za kupinga tabia ya ubinafsi wa viongozi barani Afrika. Gazeti hilo limetilia maanani katika makala yake kuwa idadi ya watu wanaoipinga tabia ya viongozi ya kujinufaisha inaongezeka barani Afrika.

Wananchi wakiandamana nchini Nigeria kupinga kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta.
Wananchi wakiandamana nchini Nigeria kupinga kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta.Picha: dapd

Gazeti hilo linaeleza kuwa mishahara ya wanasiasa inazidi kuwa mikubwa barani Afrika licha ya kuongezeka kwa umasikini. Licha ya mishahara yao mikubwa, wanasiasa hao wanataka malipo makubwa zaidi pamoja na marupurupu zaidi. Kutokana na tabia ya wanasiasa hao, wananchi sasa wanajitokeza na kupinga, nchini Kenya, Ghana, Nigeria na Afrika Kusini.

Gazeti la "Neues Deutschland" limeripoti kwamba wananchi hao wanataka wabunge na wanasiasa wengine wadhibitiwe. Gazeti hilo limetoa mfano wa Kenya. Nchi hiyo ina wabunge zaidi ya 200, mawaziri 40 na naibu mawaziri 52. Kila mbunge anapokea msharara unaofikia Euro 9,000 na posho ya 6,000 pamoja na nyumba ya bure na marupurupu mengine. Mshahara wa waziri wa Kenya ni Euro11,000 kwa mwezi. Rais mwenyewe analipwa Euro 18,000 kwa mwezi! Hata hivyo gazeti la "Neues Deutschland" linafahamisha kuwa Kenya siyo nchi pekee barani Afrika ambako wanasiasa wanajilipa mishahara mikubwa sana. Hali ni hiyo hiyo nchini Afrika Kusini, Nigeria, Ghana na Namibia.

Mapambano dhidi ya njaa

Jarida la Focus wiki hii linazungumzia juu ya harakati za kupambana na njaa barani Afrika kwa kuwasaidia mafalahi - wakulima wodogo wadogo. Jarida hilo limemkariri mfadhili mkubwa wa misaada, mwenyekiti wa Wakfu wa "Melinda na Bill Gates" akisema kuwa Wakfu huo unakusudia kuwasaidia wakulima wa Afrika katika juhudi za kupambana na wadudu waharibifu, ukame na magonjwa ya mimea.

Bill Gates amesema katika mahojiano na jarida la Focus kwamba wakfu wake utawasaidia wakulima katika juhudi za kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani.

Mwandishi:Mtullya Abdu/ Deutsche Zeitungen

Mhariri:Josephat Charo