1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya25 Mei 2014

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya Boko Haram, mkakati mpya wa Ujerumani juu ya Afrika na juu ya madhara yanayoweza kutokea kwa Afrika ikiwa Marekani na Umoja wa Ulaya zitausaini mkataba wa biashara huria

https://p.dw.com/p/1C6ON
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: DW

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" baa la Boko Haram nchini Nigeria halionyeshi dalili ya kwisha haraka wakati watu nchini humo sasa wanaishi na hofu kubwa.

Gazeti hilo limeandika kwamba viongozi wa Nigeria wanazidi kubwana.Ghadhabu miongoni mwa wananchi inaongezeka nchini Nigeria kutokana na kile kinachoonekana kuwa kushindwa kwa serikali hiyo kuwakabili magaidi wa Boko Haram. Kundi hilo la Waislamu wenye itikadi kali linazidi kujitandaza nchini Nigeria. Ingawa, hali ya hatari imetangazwa katika majimbo ya migogoro, Boko Haram bado wanaweza kufanya mashambulio kwa kadri wanavyopenda katika majimbo mengine.

Gazeti la"Berliner pia limeandika juu ya Boko Haram na linasema kwamba serikali ya Nigeria imezidiwa na haina nguvu mbele ya magaidi hao.Gazeti hilo linaeleza kwamba mashambulio yaliyofanywa na magaidi hao katika mji wa Jos yamethibitisha mapema wiki hii kwamba serikali ya Nigeria imezidiwa.

Mwongozo mpya wa Ujerumani juu ya Afrika

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linaizingatia sera mpya ya Ujerumani juu ya Afrika. Sera hiyo ni matokeo ya mjadala uliofanyika mapema mwaka mwaka huu baina ya Rais wa Ujerumani ,Joachim Gauck, Waziri wa mambo ya nje Frank-Walter Steinmeier na Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen.

Gazeti la "Der Tagesspiegel "linaeleza kwamba baada ya wizara za maendeleo, kilimo na uchumi kukubaliana, Ujerumani imeupitisha mwongozo mpya wa ushirikiano baina yake na bara la Afrika.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema ,katika msingi wa mwongozo huo Ujerumani italenga shabaha mbili. Katika upande mmoja Ujerumani itaendeleza ushirikiano na Afrika kwa kuyalenga maeneo fulani ya kuyaunga mkono na katika upande mwingine Ujerumani itashirikiana na nchi za Afrika katika kuikabili migogoro kwa haraka zaidi kuliko ambavyo imekuwa hadi sasa. Katika msingi wa mwongozo mpya juu ya Afrika, Ujerumani inaitilia maanani migogoro inayoikumba Afrika,ambayo pia inaweza kuliathiri bara la Ulaya kama vile uharamia,ugaidi na ukimbizi.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linatilia maanani kwamba sera mpya ya Ujerumani juu ya Afrika inahusu hasa masuala ya maendeleo.Hata hivyo gazeti hilo linaeleza kwamba Ujerumani itawasiliana na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa katika kuitekeleza sera hiyo.

Bara la Afrika linastawi vizuri kiuchumi

Gazeti la "Berliner "pia limeandika juu ya mwongozo mpya wa Ujerumani juu ya Afrika.Gazeti hilo linatilia maanani kwamba bara la Afrika ,katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara linastawi vizuri kiuchumi .Ustawi huo unafikia asilimia kati ya tano hadi 10. Gazeti hilo linaeleza kuwa bara la Afrika pia lina utajiri mkubwa wa mali asilia kama vile mafuta na madini. Lakini gazeti la "Berliner" linauliza jee Afrika inaitumia fursa iliyonayo?

Afrika itaingia hasara kutokana na mkataba wa Marekani na Umoja wa Ulaya

Marekani na Umoja wa Ulaya zinaendelea na mazungumzo juu ya kuufikia mkataba wa kuuanzisha ukanda wa biashara huru baina yao. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "Neues Deutschland" Katika makala iliyochapishwa na gazeti hilo Rolf- Henning Hintze anasema kuwa mkataba huo utaziathiri nchi zinazoendelea. Rolf-Henning Hintze anaeleza katika makala yake kuwa nchi za Afrika zitapata hasara kubwa ya fedha kutokana na mkataba huo.

Mkataba huo baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani maana yake ni kuondolewa ushuru baina ya pande mbili hizo. Bidhaa kutoka nchi kama Guinea na Ivory Coast zitagubikwa na bidhaa kutoka Marekani na hasa zile za pamba.

Nchi nyingine zitakazoathirika na mkataba wa biashara huru baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya ni pamoja na Uganda na Tanzania ingawa nchi hizo zinaweza kupunguza hasara kwa kuziuza bidhaa zao kwenye masoko ya China na Australia.

.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef