1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya27 Juni 2014

Wiki hii magazeti ya Ujerumani pamoja na masuala mengine yameandika juu ya mkasa wa mwanamke wa Sudan ambae hapo awali alihukumiwa adhabu ya kifo.

https://p.dw.com/p/1CRis
Mwanamke wa Sudan Mariam Ibrahim pamoja na watoto ,mumewe na ndugu zake
Mwanamke wa Sudan Mariam Ibrahim pamoja na watoto, mumewe na ndugu zakePicha: picture-alliance/AA

Gazeti la "Süddeutsche" limeandika juu ya mkasa wa mwanamke wa Sudan, Mariam Ibrahim ambae hapo awali alihukumiwa adhabu ya kifo kwa kile kilichoitwa kosa la kujitoa kwenye Uislamu na kuingia katika Ukristo.

Gazeti hilo linatuarifu kwamba mama huyo mwenye umri wa miaka 27 alizaliwa na baba mwislamu na mama mkristo kutoka Ethiopia. Lakini baadae aliamua kuolewa na mkristo ambaye ni raia wa Marekani. Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya kiislamu mama huyo ni mwislamu kutokana na nasaba ya baba yake ,na kwa hivyo haruhusiwi kujitoa kwenye uislamu. Mahakama ilimhukumu adhabu ya kifo na kutandikwa mijeledi mia moja.

Shinikizo la kimataifa lamsaidia Mariam Ibrahim

Lakini mkasa wa mama huyo ulimalizika kwa faraja baada ya kupata habari kwamba rufani yake ilikubaliwa. Sasa mama huyo Mariam Ibrahim yupo huru.Gazeti la "Süddeutsche" linasema mama huyo ameponyoka adhabu ya kifo kutokana na shinikizo la kimataifa.

Joseph Kony yuko Sudan ?

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii limeandika juu ya juhudi zinazofanywa za kumsaka kiongozi wa kundi la wauwaji la LRA la Uganda Joseph Kony.Gazeti hilo linaeleza kuwa kwa miaka mingi sasa vikosi maalumu vya nchi za Afrika na Marekani vimekuwa vinamsaka mtu huyo.

Gazeti hilo linadai kwamba wanaomsaka wanajua kwamba yuko Sudan. Lakini kwa kuwa wanajeshi hao maalumu kutoka Marekani hawashirikiani na Rais Omar al-Bashir, hawawezi kuingia Sudan .Na kwa hivyo wanamsaka katika nchi nyingine!

Wayahatarisha maisha ili kufika Ulaya

Watu zaidi na zaidi wanaondoka Afrika kwa njia ya kuyahatarisha maisha yao ili kufika barani Ulaya lakini aghalabu wanapofika barani Ulaya maisha yao yanakuwa ya mashaka. Hizo ni habari zilizoandikwa wiki hii na gazeti la "Stern"

Maradhi ya Ebola yaripuka Afrika magharibi

Na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaripoti juu ya kuripuka maradhi ya Ebola katika nchi za Afrika magharibi. Gazeti hilo linasema virusi vinavyoyasababisha maradhi hayo haviwezi kudhibitiwa na nchi hizo. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaarifu zaidi kwamba maradhi ya Ebola yamelikumba eneo lote la Afrika magharibi na kwa mujibu wa Shirika la misaada la madaktari wasiojali mipaka, nchi za sehemu hiyo haziwezi kuudhibiti ugonjwa huo.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukuu Mkuu wa madaktari wasiojali mipaka nchini Guinea ,Bart Janssens akisema kwamba idadi ya watu wanaoambukizwa virusi vya ugonjwa huo ni kubwa sana. Gazeti hilo limearifu kwamba nchi zilizofikwa na maradhi hayo ni hasa,Liberia,Sierra Leone na Guinea.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeinukuu taarifa ya Shirika la Afya Duniani,WHO inayosema kuwa watu 350 wameshakufa nchini Guinea tokea baa hilo liripuke mwanzoni mwa mwaka huu.

Wanajeshi wa Ujerumani kuendelea kusaidia nchini Mali

Bunge la Ujerumani liliamua Jumatano iliyopita kulirefusha jukumu la wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali.Gazeti hilo linaarifu kwamba wanajeshi wa Ujerumani waliopo nchini Mali wataendelea kuwapo katika nchi hiyo kwa mwaka mmoja zaidi kulitekeleza jukumu la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Idadi kubwa ya wabunge wa Ujerumani waliuunga mkono uamuzi huo. Ujerumani imechangia jumla ya wanajeshi 230 katika jeshi la Umoja wa Mataifa. 172 wapo nchini Mali.

Gazeti la "die tageszeitung" linakumbusha kwamba wapiganaji wanaoifuata itikadi kali ya kiislamu waliiteka na kuidhibiti sehemu kubwa ya Mali mwishoni mwa mwaka wa 2012 kabla ya kurudishwa nyuma na majeshi ya Ufaransa.Kwa mujibu wa gazeti hilo wanajeshi wa Ujerumani wanatoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Abdul-Rahman.