1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya7 Desemba 2014

Wiki hii magezeti ya Ujerumani yamechapisha ripoti na makala juu ya harakati za kupambana na maradhi ya Ebola . Pia yamechpisha habari juu ya mauaji yaliyofanywa na magaidi wa al-Shabaab nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/1E0PI
Wanajeshi wa Ujerumani kusaidia katika juhudi za kupambana na Ebola
Wanajeshi wa Ujerumani kusaidia katika juhudi za kupambana na EbolaPicha: picture-alliance/dpa/Pilick

Gazeti la "Der Tagespiegel" limeandika juu ya mchango wa Ujerumani katika harakati za kupambana na maradhi ya Ebola.Gazeti hilo linaarifu kwamba jeshi la Ujerumani linawapeleka askari katika nchi za Afrika magharibi ili kusadia katika juhudi za kuyakabili maradhi ya Ebola. Kwa mujibu wa habari ,wanajeshi 50 wa Ujerumani kwa sasa wapo katika nchi za Afrika magharibi.

Gazeti hilo la "Der Tagespiegel" pia limeripoti juu ya ndege iliyotengezwa maalumu kwa ajili ya kuwasafirishia watu walioambukizwa virusi vya Ebola.

Ndege hiyo iliyotolewa na shirika la ndege za abiria la Lufthansa kwanza itawarudisha nchini Ujerumani wasaidizi wote watakaopatikana na bahati mbaya ya kuambukizwa ugonjwa wa Ebola. Ndege hiyo itahudumu kama kituo cha kuwatengea watu walioambukizwa, kabla ya kupekewa hospitali.

Kuripuka kwa Ebola kunaaathiri uzalishaji wa chakula

Gazeti la "Berliner Zeitung" limemnukuu mtaalamu wa Umoja wa Mataifa Kanayo Nwanze akiitaka jumuiya ya kimataifa ijiandae vizuri zaidi katika kupambana na ugonjwa wa Ebola.Mtaalamu huyo ametahadharisha juu ya uwezekano wa kupungua uzalishaji wa mazao ya kilimo na hivyo kusababisha baa la njaa katika nchi za Afrika magharibi.

Magaidi wa al-Shaabab wauawa tena nchini Kenya

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limechapisha ripoti juu ya mauaji yaliyofanywa na magaidi wa al-Shaabab nchini Kenya .Magaidi hao waliawaua wafanyakazi 36 kaskazini mashariki mwa Kenya usiku wa kuamkia siku ya Jumanne . Kutokana na mashambulio hayo Rais Uhuru Kenyatta alichukua hatua kali.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linafahamisha kwamba Rais Kenyatta amefanya mabadiliko katika uongozi wa wizara ya mambo ya ndani. Gazeti hilo limemnukuu Kenyatta akisema kuwa kuna vita dhidi ya Kenya , na wananchi wake, na kwamba lazima Kenya ishinde katika vita hivyo.


Gazeti la "Franfurter Allgemeine" liinasema kwamba mara tu baada ya kutokea mashambulo hayo Rais Kenyatta alimwachisha kazi waziri wake wa mambo ya ndani Ole Lenku alieutumikia wadhifa huo kwa muda wa miezi mitano tu.Gazeti hilo pia limefahamisha kwamba Mkuu wa Polisi ya Kenya David Kimaiyo pia ameondolewa kwenye wadhifa wake.

Katika ripoti yake gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limesema mabadiliko yaliyofanyika katika wizara ya mambo ya ndani nchini Kenya yanaonyesha jinsi Rais Kenyatta alivyojizatiti katika kuukabili ugaidi nchini mwake.

Uganda yakusudia kulibinafsisha ziwa Victoria

Sindano ya uzima kwa ziwa Victoria.Hizo ni habari zilizondikwa na gazeti la "die tageszeitung" mnamo wiki hii. Gazeti hilo limearifu kwamba kutokana na hali mbaya ya ziwa hilo idadi ya samaki inazidi kupungua na hivyo mapato ya wavuvi pia yanapungua katika nchi zote tatu zinazopakana na ziwa hilo,Kenya ,Tanzania na Uganda. Gazeti la "die tageszeitung" linatufahamisha juu ya mpango wa serikali ya Uganda wa kuwasaidia wavuvi.

Gazeti hilo linaarifu kwamba kuanzia mwaka 2005 idadi ya samaki imepungua kwa asilimia 80 kwenye ziwa Victoria. Hali hiyo inaathiri mapato ya watu wanaotegemea shughuli za uvuvi ili kuendeshea maisha yao. Kutokana hali hiyo, gazeti la die" tageszeitung" linatufahamisha kwamba serikali ya Uganda ina mpango wa kulibinafsisha ziwa Victoria. Waekezeji vitega uchumi binafsi wataanzisha sehemu za kuzalishia samaki ili kuongeza idadi yao.


Katika kuutekeleza mradi huo,serikali ya Uganda imetoa mwito kwa wafanya biashara wazawa na kutoka nje waekeze vitega uchumi.

Gazeti la "die tageszeitung" linatilia maanani katika makala yake kwamba mauzo ya samaki katika nchi za nje yamekuwa yanaiingizia Uganda kiasi cha Euro Milioni mia moja kila mwaka tokea mwaka wa 2010. Mauzo ya samaki nje ya nchi yamethibiti kuwa tawi muhimu katika uchumi wa Uganda linasema gazeti hilo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Saumu Yusuf