1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wakombolewa Nigeria

10 Mei 2015

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yanakumbusha juu ya historia ya Burundi katika muktadha wa mgogoro wa kikatiba unaondelea nchini humo hivi sasa.Pia yameandika juu ya wanawake waliokombolewa na jeshi nchini Nigeria.

https://p.dw.com/p/1FNXt
Jeshi la Nigeria lawakomboa wasichana
Jeshi la Nigeria lawakomboa wasichanaPicha: picture-alliance/dpa/EPA/Nigerian Army

Katika makala yake gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linazungumzia juu ya mgogoro wa kisiasa nchini Burundi uliosababishwa na uamuzi wa Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu wa urais kinyume na katiba.

Gazeti hilo limeandika kwamba hutokea mara kwa mara barani Afrika,kwamba kiongozi wa nchi anang'ang'ania mamlaka. Na kwa ajili hiyo anakuwa tayari kuipinda katiba ya nchi kwamaslahi yake.

Matukio ya sasa yakumbusha maafa ya miaka ya nyuma
Lakini gazeti la "Süddeutsche " linasema ikiwa jambo kama hilo linatokea katika nchi ndogo kama Burundi, watu mara moja wanaanza kuvikumbuka vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini humo. Watu zaidi ya mia tatu alfu walikufa kutokana na vita hivyo.

Gazeti la "Südeutsche" limeinuku taarifa ya shirika la Msalaba Mwekundu inayosema watu zaidi ya 18 wameshauawa nchini Burundi katika siku za hivi karibuni. Gazeti hilo limeeleza kuwa maalfu ya watu wanajitpkeza katika mitaa ya mji mkuu Bujumbura na kushiriki katika maandamano ya kuupinga uamuzi wa Rais Nkurunziza.

Gazeti la "Südeutsche" linasema polisi nchini Burundi wanatumia nguvu katika kujaribu kuwadhibiti waandamanaji. Na gazeti la "Berliner Zeitung" linasema Polisi wa Burundi wanawapiga risasi raia wanaofanya maandamano.

Wanawake na wasichana wakombolewa nchini Nigeria

Gazeti la "Der Tagesspiegel" wiki hii limeandika juu ya matukio ya nchini Nigeria.Linasema mabadiliko yameanza kuonekana nchini humo baada ya uchaguzi .Gazeti hilo linaeleza kwamba jeshi la Nigeria limeanza kuonyesha dhamira ya kweli katika kupambana na magaidi wa Boko Haram baada ya kufanyika uchaguzi .


Gazeti la "Der Tagesspiegel" linatilia maanani kwamba mnamo kipindi cha wiki moja tu wanajeshi wa Nigeria wameweza kuwakomboa jumla ya wanawake na wasichana 700 waliokuwa wametekwa nyara na magaidi wa Boko Haram.


Gazeti hilo limeikariri taarifa ya Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International inayosema kwamba mnamo kipindi cha mwaka mmoja na nusu kilichopita,magaidi wa Boko Haram waliwateka wanawake na wasichana zaidi ya 2000 nchini Nigeria. Gazeti hilo pia limemnukulu msemaji wa jeshi la Nigeria akielezea matumaini kwamba wanawake na wasichana zaidi watakombolewa.

Gazeti la "Frankfurter" Allgemeine" limechapisha taarifa juu ya uamuzi wa Senegal wa kuwapeleka askari wake 2100 nchini Yemen ili kuilinda miji mitakatifu ya kiislamu. Gazeti hilo linafahamisha zaidi kwamba Senegal itajiunga na majeshi ya nchi kadhaa yanayoongozwa na Saudi Arabia katika kupambana na waasi wa Kihouthi nchini Yemen.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnuku Waziri wa mambo ya nje wa Senegal Mankeur Ndiaye akieleza kwamba lengo ni kuilinda miji mitakatifu ya Mecca na Madina. Gazeti hilo limeeleza kwamba Senegal imeupitisha uamuzi huo ili kuyakubali maombi ya Mfalme wa Saudi Arabia Nchi kadhaa,miongoni mwao, Morocco,Sudan na Misri zimeungana na Saudi Arabia katika kupambana na waasi wa Kihouthi nchini Yemen.

Chama cha upinzani chapinga uamuzi huo


Hata hivyo gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linafahamisha kwamba kiongozi wa chama cha upinzani nchini Senegel Modou Diagne ataupinga uamuzi huo bungeni. Amesema Saudi Arabia haitishiwi na yeyote, Gazeti hilo pia limekumbusha kwamba katika miaka ya nyuma Senegel ilikuwa inapatiwa msaada wa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga miundo mbinu nchini.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen

Mhariri: Yusuf Saumu