1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini Gbagbo tu afikishwe mahakamani ?

1 Februari 2016

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya mashtaka yanaomkabili aliekuwa Rais wa Côte d'Ivoire Laurent Gbagbo ,pia yameripoti juu ya uchaguzi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/1Hmfs
Aliekuwa Rais wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo
Aliekuwa Rais wa Cote d'Ivoire Laurent GbagboPicha: picture-alliance/dpa/P. Dejong

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya mashtaka yanaomkabili aliekuwa Rais wa Côte d'Ivoire Laurent Gbagbo ,pia yameripoti juu ya uchaguzi katika Jamhuri ya Afrika ya kati.

Aidha yanauliza iwapo ni sahihi kutoa msaada wa fedha kuwafadhili bikira kama njia ya kuwaepusha wasichana wa shule na ujauzito?

Gazeti la "die tageszeitung" linayazingatia mashtaka yanaomkabili aliekuwa Rais wa Côte d'Ivoire Laurent Gbagbo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague. Gbagbo ni mtu wa kwanza aliewahi kuwa Rais, kufikishwa kwenye mahakama hiyo kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Gazeti la "die tageszeitung" linasema majeraha bado hayajapona nchini Côte d'Ivoire. Linasema Gbagbo amefikishwa mahakamani lakini wapinzani wake bado.

Gazeti la "die tageszeitung" limefanya mahojiano na mama mmoja ,Kadi Coulibaly aliepigwa wakati wa uchaguzi. Coulibaly ameliambia gazeti hilo kwamba alilazimishwa kuvua nguo. Baada ya hapo alipigwa vibaya, na ilidibi apelekwe hospitali.

Mama huyo ameliambia gazeti la " die tageszeitung" kwamba alipigwa na wafuasi wa mshindi wa uchaguzi, yaani Rais Alassane Ouattara.

Gazeti hilo limemnukulu Kadi Coulibaly akisema hafahamu kwa nini,ni Gbagbo tu aliefikishwa mahakamni mjini The Hague! Gazeti la "die tageszeitung" limekumbusha kwamba hadi wakati wa kukamatwa kwa Gbagbo watu zaidi ya 3000 walikuwa wameshakufa kutokana na ghasia nchini Côte d'Ivoire .

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linazungumzia juu ya chaguzi zinazofanyika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Gazeti hilo linasema fedha zinatumika kwa ajili ya kununulia kura na linatilia maanani kwamba ni vigogo wa hapo zamani wanaoendelea kuwika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati .

Gazeti hilo linasema yeyote atakaechaguliwa kuwa Rais atapaswa kufanya kazi na " bunge la zamani."

Juhudi za kuwaepusha wasichana na ujauzito

Gazeti la "Berliner " limeripoti kwamba, ili msichana apate nafasi ya kufanya masomo ya chuo kikuu , katika jimbo la Kwa Zulu nchini Afrika Kusini anapaswa kuthibitisha kwamba yeye bado hajaguswa kimapenzi na mwanamume!

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Afrika Kusini
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel nchini Afrika KusiniPicha: picture-alliance / dpa

Gazeti hilo linafahamisha kwa nini Mkuu wa wilaya ya Uthukela katika jimbo la Kwa - Zulu ameuanzisha mradi huo.

Wilaya ya Uthukela katika jimbo hilo, imekumbwa na kiwango kikubwa sana cha maambukizi ya virusi vya ukimwi.Pamoja na hatari hiyo, idadi kubwa ya wasichana wanayakatiza masomo yao kutokana na ujauzito. Mkuu wa wilaya ya Uthukela amekaririwa akisema , lengo la mradi huo ni kutambua juhudi za wasichana wa shule wanaojiepusha na vitendo vya ngono.


Hata hivyo gazeti linasema mradi huo umesababisha malalamiko makubwa. Watetea haki za binadamu nchini Afrika Kusini wamenukuliwa na gazeti la "Berliner" wakisema kuwa mradi huo unahujumu uhuru wa faragha wa wasichana.

Gazeti hilo pia limewanukulu wataalamu wakitanabahisha kwamba kutokuwa bikira hakuna maana kwamba msichana alikuwa mpotevu.

Katika taarifa yake gazeti la "Berliner " limekumbusha juu ya takwimu za kutisha kuhusu vitendo vya ngono nchini Afrika Kusini.Linafahamisha kwamba thuluthi moja ya wasichana wanaguswa kingono kabla ya kumaliza masomo ya shule ya upili.


Gazeti la "die tageszeitung" limebainisha katika utafiti wake kwamba wakimbizi wa Afrika wanatumiwa kama bidhaa za kubadilishwa .

Gazeti hilo limeripoti juu ya mkasa wa mkimbizi mmoja kutoka Eritrea aliekimbilia Israel. Linasema kwa bahati mbaya mkimbizi huyo, Aman Beyen alijikuta yuko jela nchini Israel.

Gazeti la "die tageszeitung" linafahamisha kwamba sasa mkimbizi huyo anasubiri yamfike ,kama yale yaliyowafika wakimbizi wengine,yaani kufukuzwa Israel na kupelekwa , ama Uganda au Rwanda. Na kwa kuwapokea wakimbizi hao, nchi hizo zinapewa chochote na Israel; vifaa vya tekinolojia za kisasa na mafunzo ya kijeshi.


Gazeti la "die tageszeitung" linauliza iwapo kuna mkataba wa siri baina ya Israel na nchi hizo za kiafrika?

Mwandishi: Mtullya Abdu.

Mhariri: Daniel Gakuba