1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Daniel Gakuba
22 Machi 2019

Maafa ya dhoruba iliyozikumba nchi za Kusini Mashariki mwa Afrika ni mada zilizozingatiwa na magazeti ya Ujerumani manmo wiki hii.

https://p.dw.com/p/3FWQP
Mosambik Zyklon Idai | Zerstörung und Hilfe
Picha: Reuters/S. Sibeko

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche juu ya maafa yaliyozikumba nchi za Kusini Mashariki mwa Afrika kutokana na dhoruba Idai linasema maafa hayo ni majanga ya asili, lakini linatilia maanani kwamba wale wanaoyasababisha majanga hayo kwa kiwango kidogo ndiyo wanaokumbwa zaidi na athari zake.

Gazeti la Süddeutsche linasema juu ya maafa hayo yaliyozikumba Msumbiji, Zimbabwe na Malawi kwamba ukanda huo wa Kusini Mashariki mwa Afrika unasikika kwenye vyombo vya habari kwa nadra. Na hasa Msumbiji na Malawi zinasikika kwenye vyombo hivyo, pale tu panapofanyika chaguzi za marais. Na sasa zinaposikika habari juu ya majanga ya asili katika ukanda huo, inathibitika wazi kuwa hiyo ni sehemu iliyokumbwa zaidi na majanga hayo yanayotokana na mabadiliko ya  tabia nchi ingawa ni sehemu ambayo  haikuchangia kwa kiwango kikubwa katika  kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa.

Gazeti la Süddeutsche linasema ukanda wa  Kusini Mashariki mwa Afrika umekumbwa zaidi  na athari za majanga ya asili kwamba nchi za sehemu hiyo hazina nyenzo za kuziwezesha kuyapunguza makali ya athari za majanga hayo.

Neue Zürcher

Nalo gazeti la Neue Zürcher pia limeandika juu ya maafa hayo yaliyozikumba nchi za Kusini Mashariki mwa Afrika lakini linakumbusha yaliyokwishatokea nchini Msumbiji na linaeleza kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi masikini duniani yenye ufukwe wa kilometa 2700 ambako  pana msongamano mkubwa wa watu. Sehemu hiyo haiwezi kuhimili majanga ya asili kama  vimbunga, mafuriko, mvua kubwa na pepo kali. Miundombinu na nyumba zinajengwa kwa bei nafuu na ndiyo sababu haiwezi kustahimili hali mbaya za hewa. Mnamo mwaka 2000 mafuriko  yaliyosababishwa na kimbunga "Eline" yaliwaangamiza watu 8000 na nyumba nusu milioni ziliteketezwa.

Gazeti hilo la Neue Zürcher pia linakumbusha  kwamba mnamo mwaka 2007 kimbunga kingine kilichoitwa „Flavio" kiliteketeza nyumba zaidi  ya 130,000 na kuwalazimisha watu zaidi ya 10,000 wakose pa kukaa nchini Msumbiji, lakini linasema kiwango cha maafa ya safari hii haikijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba maafa  hayo makubwa yamewakumbuka tena masikini.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linatupeleka Uganda ambako zimepatikana taarifa kwamba watu kadhaa wamekufa baada ya kula chakula kilichokuwa na sumu. Chakula hicho kilichokuwa kimeharibika ulikuwa msaada kutoka shirika la chakula la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watu wa jimbo la Karamoja la kaskazini mashariki mwa Uganda. Uchunguzi uliofanywa umebainisha kwamba shirika hilo la Umoja wa Mataifa liligawa unga na mafuta ya kupikia kwa kaya zaidi ya 200 katika jimbo hilo la Karamoja. Watu kadhaa walikufa na wengine zaidi ya 260 walipelekwa hospitali ili kupatiwa matibabu.

Gazeti hilo la die tageszeitung limemnukuu waziri wa Uganda anayeshughulikia masuala ya wakimbizi Mussa Ecweru akisema kwamba chakula hicho kiliharibika wakati wa kupakiwa katika magunia. Gazeti hilo linasema kwa muda wa miaka zaidi ya 10 shirika la chakula la Umoja wa Mataifa, WFP limekuwa linatoa msaada wa unga wa uji katika jimbo la Karamoja la nchini Uganda. WFP inanunua unga huo kutoka nchini humo humo.

Die Zeit

Gazeti la Die Zeit ambalo wiki hii limechapisha makala kuusuta upotoshaji unaoenezwa nchini Kongo kuhusiana na harakati  za kupambana na maradhi ya Ebola na linaeleza kwamba maradhi hayo yameripuka nchini Kongo lakini inawezekana kuyadhibiti. Jambo muhimu ni kupata imani ya wananchi, sambamba na juhudi za kuyatibu kwani dawa mpya zina nguvu kubwa zaidi ya kuponyesha lakini asasi ya madaktari wasiokuwa na mipaka imesema zipo habari za kupotosha nchini Kongo juu ya maradhi ya Ebola zinazoenezwa kwa njia ya mitandao ya kijamii na hasa WhatsApp.

Gazeti hilo la Die Zeit limenukuu mfano mmoja  wa upotoshaji huo unaoenezwa kwenye mitandao kwamba sehemu fulani za mwili, za watu  wanaokufa zinachukuliwa na wasaidizi wanaotoka nje ya nchi. Uzushi huo unaenea haraka kwa njia ya WhatsApp na watu wanahofia kuwapeleka wagongwa wao kwenye vituo vya  tiba.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen