1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri:  Josephat Charo
29 Machi 2019

Mojawapo ya makala zilizoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni habari kuhusu mwalimu, mtawa wa nchini  Kenya Peter Tabichi aliyechaguliwa kuwa mwalimu bora duniani kote.

https://p.dw.com/p/3Fs2h
Vereinigte Arabische Emirate, Dubai - Ein kenianischer Lehrer für Naturwissenschaften gewann einen Preis im Wert von 1 Million Dollar
Picha: picture-alliance/J. Gambrell

Frankfurter Allgemeine 

Huenda mapinduzi makubwa yakaanza kutokea barani Afrika. Viongozi wa bara hilo walipitisha wazo la kuuanzisha mradi huo mjini Addis Ababa. Na ikiwa utaidhinishwa na zaidi ya nchi 22 kwenye mkutano wa kilele wa nchi za Afrika utakaofanyika mnamo mwezi julai, Mkataba wa biashara huru utaanza kutekelezwa. Hata hivyo gazeti la Frankfurter Algemeine linasema bado yapo mashaka mengi na kwamba tatizo kubwa ni uhafifu  wa miundombinu. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba mpaka leo bado zipo barabara za tangu enzi ya ukoloni katika sehemu fulani na linaendelea kueleza:

Matatizo mengine ni ukosefu wa dhamira ya utekelezaji, na kiwango cha chini cha uwezo wa kuziongezea thamani bidhaa. Nchi za Afrika kwa kiwango kikubwa zinauza nje malighafi bila ya  kuziongezea thamani. Lakini gazeti la Frankfurter Algemeine linasema licha ya matatizo hayo bara la Afrika limekuwa muhimu katika miaka ya hivi karibuni. Gazeti hilo linasema matatizo ya Afrika yanaweza kutatuliwa na waafrika wenyewe, na ndiyo sababu kuanzishwa kwa ukanda wa biashara huru ni mwanzo mzuri. 

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung wiki hii llimeandika juu ya hatua ya Ujerumani ya kuweka mwongozo mpya katika sera yake juu ya Afrika. Kulingana na mwongozo huo Ujerumani itakuwa mshirika katika juhudi za kuudumisha ushirikiano wa mataifa yote duniani. Ujerumani katika mwongozo huo mpya inalizingatia bara la Afrika kuwa mshirika muhimu katika juhudi za kuleta amani na usalama duniani na pia katika juhudi za kupunguza na kudhibiti uundaji silaha. Na kutokana na tathmini hiyo mpya, Ujerumani inaitambua sura nyingine ya Afrika, na siyo tena ile ya bara la migogoro.

Neue Zürcher

Nalo gazeti la Neue Zürcher linatupasha habari juu ya mradi mkubwa wa maendeleo nchini Ethiopia, na linatuambia kwamba mradi mpya wa reli inayoziunganisha Ethiopia na bahari ya Shamu uliozinduliwa mwezi Januari mwaka uliopita ni wa treni ya kwanza ya umeme barani Afrika itakayoziunganisha nchi mbili za Afrika, Ethiopia na Djibouti. Treni hiyo itakata mbuga, mabonde na milima, umbali wa kilometa 750 kutoka mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa hadi bandari ya Djibouti kwenye bahari ya Shamu. Mkopo wa Euro bilioni tatu, kutoka China ulihitajika kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo.

Reli hiyo pia ni muhimu kwa biashara ya ndani nchini Ethiopia. Asilimia 70 ya biashara ya nje ya Ethiopia inapitia kwenye bandari ya Djibouti. Ni reli yenye manufaa makubwa kwa watu milioni 100  wa  Ehtiopia.Hata hivyo yapo matatizo. Gazeti la Neue Zürcher linaeleza kwamba ujenzi wa reli hiyo umeleta mivutano. Wakulima waliochukuliwa ardhi zao hawakulipwa fidia vizuri. Badala yake fedha ziliingia katika mifuko ya mafisadi. La kutilia maanani zaidi ni kwamba wakulima hao hasa wako kwenye jimbo la Oromo.

Ingawa Waoromo ndio wengi zaidi nchini Ethiopia wamekuwa wanawekwa mbali na hatamu za uongozi, hadi hivi karibuni, alipochaguliwa waziri mkuu Abiy Ahmed anayetoka kwenye kabila hilo. Kwa Waoromo, mradi huo wa reli unamaanisha maonevu wanayofanyiwa na makabila mengine pamoja na makampuni ya kimataifa.

die tageszeitung

Habari juu  ya mwalimu, mtawa wa nchini  Kenya Peter Tabichi aliyechaguliwa kuwa mwalimu bora duniani kote. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti hilo  la die Tageszeitung. Mwalimu huyo anawafundisha watoto 58  katika darasa moja. Mbali na kufundisha masomo ya sayansi, Peter Tabichi anatoa asilimia 80 ya mshahara wake kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo. Alitunukiwa tuzo ya "Global Teacher Prize”  ya donge la dola milioni moja za kimarekani.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen